Serikali yawataka wazazi kuwakataza watoto kutazama Squid Game
Na WANGU KANURI
SERIKALI kupitia Bodi ya Kusimamia na Kukadiria Uainishaji wa Filamu nchini (KFCB) imewashauri wazazi kuwakataza watoto wao kutazama filamu maarufu ya Squid Game.
Akiwahutubia wanahabari Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo Bw Christopher Wambua alieleza kuwa filamu ya Squid Game inapaswa kutazamwa tu na watu wazima pekee.
“Kulingana na Netflix, filamu hiyo inapaswa kutazamwa tu na mtu mwenye umri wa miaka 18. Hii ni kwa sababu, filamu hiyo ina maonyesho yenye kuchochea vurugu, mapenzi na ngono. Ni muhimu kufahamu kuwa filamu hiyo inapaswa kutazamwa na watu wazima peke yake,” akaeleza Bw Wambua.
Hatua hiyo ya KFCB inajiri baada ya baadhi ya wazazi kuwasilisha malalamishi yao kufuatia uigizaji halisia wa filamu hiyo kwenye shule na nyumbani.
Bw Wambua alieleza kuwa uigizaji wa Squid Game hata kama unaonekana kama hauna hatia unaweza ukachochea vurugu na visa vya kudorora kwa tabia kama inavyoonyeshwa kwenye filamu hiyo.
“Mnamo 2021, mwanarika mmoja alikiri kuwaua wazazi wake na ndugu zake baada ya kuathiriwa na filamu moja iliyoitwa ‘Killing Eve.’ Nyuma kidogo mwaka wa 2017, mchezo mwingine maarufu ulioitwa ‘Blue Whale’ ulidaiwa kuchangia visa vya kujitoa uhai kwa watoto katika maeneo tofauti ya dunia ikiwemo nchi ya Kenya,” akasema Bw Wambua.
Squid Game, iliyotolewa Septemba mwaka huu, ina asili ya Kikorea lakini imetiwa sauti kwa lugha ya Kiingereza.
Kwa mtazamo huo, KFCB imewashauri wazazi kuwa waangalifu na kuangaza kile watoto wao wanatazama kupitia vyombo vya habari.
Isitoshe, KFCB ilitangaza kushirikiana na Netflix katika kuwaelimisha wazazi na walimu kuhusu njia za kuhakikisha kuwa wamedhibiti kinachotazamwa na watoto wao.
Bodi hiyo iliwaandikia ujumbe wakuu wa kampuni ya Google ikiwaomba kuondoa kwenye YouTube sehemu za Squid Game zilizo na matukio yaliyo na maonyesho ambayo yanaweza kuwadhuru watoto.
Next article
Vyama vidogo vinachochea chuki na ukabila, Ruto adai