Connect with us

General News

Shahidi apandwa na hasira akidaiwa si mwaminifu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Shahidi apandwa na hasira akidaiwa si mwaminifu – Taifa Leo

ICC: Shahidi apandwa na hasira akidaiwa si mwaminifu

NA VALENTINE OBARA

SHAHIDI wa kwanza wa upande wa mashtaka kwa Mahakama ya Kitaifa ya Uhalifu (ICC) katika kesi dhidi ya wakili Paul Gicheru, alipandwa na mori wakati wakili wa mshtakiwa alimtaka kuthibitisha uaminifu wake Jumatano.

Bw Michael Karnavas anayemwakilisha Bw Gicheru katika kesi hiyo inayohusu madai kwamba mshtakiwa alihusika katika kuhonga mashahidi wajiondoe kwenye kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 iliyomkumba Naibu Rais William Ruto, alikuwa anauliza maswali mengi ya kutaka kuthibitishia mahakama kwamba shahidi aliyeletwa si mwaminifu.

“Wakili anaendelea kunirejelea kama mwongo na siridhishwi na mwelekeo wake wa kuuliza maswali. Naomba ulinzi wa mahakama. Naomba wakili aheshimu uadilifu wangu kwa sababu kama ningekuwa mwongo, taarifa zote ambazo nimeleta katika mahakama hii hazingekuwa hapa. Taarifa nilizoleta hapa zina msingi ndiposa tunazijadili leo,” shahidi huyo aliyebanwa jina kwa ulinzi wake, akasema kwa ukali.

Hata hivyo, Jaji Miatta Maria Samba, alimshauri awe mtulivu na kujibu maswali aliyoulizwa kwa vile hayakukiuka kanuni za mahakama hiyo.

“Naomba utilize hasira. Nina hakika wakili hataki kutilia shaka uadilifu wako kwa hivyo tulia ujibu maswali na mambo yatakuwa sawa,” akasema jaji.

Bw Karnavas aliibua maswali hayo kwa msingi kuwa, awali shahidi huyo alisemekana alikiri mahakamani kwamba kuna wakati alisema jambo moja alipohojiwa ingawa alikuwa amenuia kusema kivingine.

Bw Gicheru anashtakiwa kwa madai ya kumwakilisha Dkt Ruto katika kutafuta na kuhonga mashahidi ili wajiondoe kwenye kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo naibu rais alikuwa ameshtakiwa pamoja na mtangazaji wa redio Joshua Sang.

Imedaiwa kuwa, mshtakiwa alishirikiana na wengine akiwemo marehemu Meshack Yebei, kuwatafuta mashahidi ambao walilipwa mamilioni ya pesa huku wengine wakitishiwa maisha ili wasishirikiane na upande wa mashtaka kuendeleza kesi ya Dkt Ruto.