Shirika ladai kuwepo kwa jela za siri Kenya
UTEKAJI NYARA | Ripoti yasimulia mateso ambayo walioponyoka mikononi mwa watekaji wao wakiwa hai walipitia. Wengi wa wanaotekwa huuawa
NA WAANDISHI WETU
WASIWASI umeibuka kuhusu kuwepo kwa jela za siri nchini ambazo hutumiwa kutesa watu wanaotoweka kwa njia zisizoeleweka, kisha baadhi yao kupatikana baadaye wakiwa wameuawa.
Visa vya watu kutekwa nyara nchini kwa njia tatanishi na baadaye kupatikana wameuawa huku wachache wakikataa kuzungumzia masaibu yao wanapopatikana wakiwa hai, vimekuwa vikiongezeka kila mara.
Bw Taimur Kariuki Hussein, 39, ambaye ni mkazi wa Watamu, Kaunti ya Kilifi, alitoweka mwaka uliopita na kurudi nyumbani baada ya kuzuiwa kwa miezi sita.
Sawa na wenzake ambao wamewahi kupatikana wakiwa hai, alikataa kabisa kuzungumzia aliyoyapitia huku ikisemekana alionywa kwamba angerudishwa kule alikokuwa amezuiwa iwapo atafungua kinywa kusema chochote kuhusu masaibu yake. Familia yake ilieleza k wa, alipewa nauli ya kurejea nyumbani na watekaji wake baada ya kuachwa katika Kaunti ya Nairobi, mnamo Novemba 27, mwaka uliopita.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika, sasa limechapisha ripoti inayosimulia maelezo ambayo baadhi ya waathiriwa walitoa kuhusu masaibu yao.
Miongoni mwa visa hivyo ni kuhusu Sombwana Athman, Aisha Omar na Khalid Hashim ambao walidaiwa kukamatwa kutoka nyumbani kwao Miyabogi, Kaunti ya Lamu mnamo Januari 14, 2020. Ilisemekana walikamatwa na watu waliokuwa wamevaa sare za polisi, kisha mwezi mmoja baadaye waliachiliwa huru.
“Tulitekwa usiku wa manane, tukiwa tumefumbwa macho na kusafirishwa kwa gari kwa saa nyingi. Tulibaki tumefungwa pingu kwenye mikono safari nzima. Nilipata alama kwenye viganja vyangu kutokana na jinsi walivyokuwa wamenifunga pingu. Ulifika wakati mikono yangu ilikufa ganzi,” anasimulia Bi Omar.
Mwenzake, Bw Hashim alifunguka jinsi alivyobanwa shingoni hadi akabaki na alama.
Mwathiriwa mwingine ambaye jina lake tunalibana kwa sababu za kiusalama, alieleza kuwa alisafirishwa kwa muda mrefu na waliposimama, alitupwa kwenye chumba chenye giza ambapo alisikia watekaji wakiitana wasaidiane kumpiga.
“Nilipigwa mateke na wakati mwingine kwa rungu. Walipogundua sijibu maswali yao walinitupa kwenye shimo ambalo nilikuwa niking’atwa na kitu, ninashuku kuwa ni mchwa. Yalikuwa maumivu ambayo sitasahau kamwe,” alieleza mwathiriwa huyo.
Mwathiriwa mwingine anasema aliumwa na mchwa hadi mwili wake wote ukavimba.
“Niliathiriwa kiwango cha kushindwa kusimama, kuketi wala kulala kwa sababu ya maumivu niliyokuwa nikipata,” akaeleza.
Kwa mujibu wa wale waliokubali kuhojiwa na watetezi wa haki za binadamu, unyanyasaji na mateso waliyopata ni kwa sababu walikosa kujibu maswali waliyoulizwa.
Walisema kuwa, mara nyingi maswali hayo yalihusu mtu ambaye walikuwa hawamjui wala hawajawahi kusikia kumhusu.
“Nililazimika kujibu maswali ambayo sikuwa na majibu yake huku nikiwa nimesimama kwenye ukingo wa shimo lililojaa mamba.
Wakati mmoja nililia nikiomba waniachilie,” akasema mwathiriwa mwingine. Wengine walithibitisha kupelekwa katika kiwanja na kuondolewa kitambaa machoni huku wakionyeshwa miili ya watu iliyooza na kutishiwa kuuawa pia kwa jinsi hizo.
Mkurugenzi wa shirika la Haki Afrika, Bw Hussein Khalid anasema kuwa maelezo hayo yanaashiria uwezekano wa kuwepo jela za siri za mateso humu nchini katika maeneo mbalimbali.
POLISI Hata hivyo, haijabainika wazi ni nani wanaosimamia sehemu hizi zinazotumiwa kutesa na kuua watu wanapotekwa nyara.
Mwaka uliopita, watu 30 walitoweka kwa njia isiyoeleweka na baadaye kupatikana sehemu mbalimbali nchini. Ijapokuwa wengi wao hulaumu polisi kwa kuhusika na visa hivyo, serikali imeshikilia mara kwa mara kuwa haihusiki.
Baadhi ya maafisa serikalini hudai kuwa kuna watu wengine wanaotekwa nyara na mahasimu wao wa kibiashara huku ikidaiwa waathiriwa wengine ‘hujipoteza’ wenyewe.
Hata hivyo, Novemba 2021, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alisema kuna baadhi ya maafisa wa polisi ambao hutumiwa na wahalifu kwa utekaji nyara ila akaondolea lawama idara ya polisi akisema maafisa wa aina hiyo hawawakilishi idara hiyo ya usalama wa taifa.
“Tabia za maafisa wachache hazifai kukubaliwa kuharibia jina idara nzima. Tutaendelea kuwaondoa wakiukaji sheria ndani ya idara ya polisi ili kuwatumia kama mfano na kukumbusha kila mtu kwamba serikali hii ni ya kiraia na haifuati imani za kuua raia wake,” akasema Dkt Matiang’i.
Alisema hayo baada ya mkutano na maafisa wa mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Shirika la Haki Africa linasema waathiriwa 22 kati ya 30 walioripotiwa kutoweka walipatikana wakiwa hai huku wanane wakiwa wameuawa.
Inahofiwa kuwa huenda kuna watu wengi zaidi ambao huwa hawaripotiwi, kwani katika miezi ya hivi majuzi, miili imekuwa ikipatikana imetupwa katika mito na misituni.
Ripoti hiyo pia inaashiria kuwa eneo la Pwani ndilo linaloongoza kwa visa hivi.
Kisa cha Juma Omar, 29, na Hamisi Mwinyi, 17, waliopatikana wamefariki Machi 6, mwaka jana ni miongoni mwao. Wawili hao wanatoka katika Kijiji cha Kibundani, Kaunti ya Kwale.
Walikuwa wameripotiwa kutoweka Februari 16, 2021, muda mfupi baada ya kudaiwa kutekwa nyara na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi. Maiti hizo zilipatikana baadaye katika Hospitali Kuu ya Pwani.
Kisa cha pili ni cha Elijah Obuong, 35, Benjamin Imbayi, 30, na Brian Oduor, 36. Watatu hao walikuwa wameripotiwa kutoweka Aprili 19, mwaka jana huko Kitengela, Kaunti ya Kajiado. Hapo awali walikuwa wameripotiwa kutoweka Kitengela baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kuwakusanya kwenye gari.
Mwili wa Bw Obuong ulipatikana katika Mto Mathioya, Murang’a huku mwili wa Imbayi ukipatikana katika mochari mjini Thika.
Next article
Kiswahili sasa kutumiwa na AU kuendeshea vikao