Connect with us

General News

Shughuli za bunge zafufuka – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Shughuli za bunge zafufuka – Taifa Leo

Shughuli za bunge zafufuka

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE shughuli za bunge zimekwamuliwa baada ya wabunge, Jumanne, Februari 1, 2022, kuipitisha hoja ya kuundwa upya kwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC).

Kabla ya kupitishwa kwa hoja hiyo, wabunge waliidhinisha hoja ya kubatilisha uamuzi wa Jumanne wiki jana ambapo wabunge wa mrengo wa muungano wa Kenya Kwanza, walichochea kukataliwa kwa majina ya wanachama saba walioteuliwa kuhudumu katika kamati hiyo muhimu.

Wale waliopendekezwa kuhudumu katika HBC ni Joyce Emanikor (Mbunge Mwakilishi wa Turkana), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Kawira Mwangaza (Mbunge Mwakilishi wa Meru), Mohamed Abdikharim Osman (Fafi), Makali Mulu (Kitui ya Kati), Mishi Mboko (Likoni) na Godffrey Osotsi (Mbunge Maalum, ANC).

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya, Februai 1, 2022 alirejesha hoja mpya lakini yenye majina yayo hayo na wabunge wakapitisha bila upinzani mkali tofauti na Jumanne, Januari 25, 2022.

“Nawaomba wabunge kupitisha majina ya wanachama hawa waliopendekezwa kuhudumu katika kamati hii muhimu. Hii ni kwa sababu wiki jana orodha hii iliangushwa sio kwa sababu ilikuwa na dosari yoyote bali ni kutokana na mivutano ya kisiasa kutoka nje ya bunge hili,” akasema Bw Kimunya ambaye ni mbunge wa Kipipiri.

Baada ya kupitishwa kwa hoja hiyo, Spika Justin Muturi aliahirisha kikao hicho ili kutoa nafasi kwa kamati ya HBC ikutane kuratibu shughuli za bunge.

“Kwa kuwa hakuna shughuli nyingine, naamuru bunge liahirishwe hadi Jumatano saa tatu na dakika 30 asubuhi. Kutakuwa na ajenda za kujadiliwa. Kwa hivyo, nawaomba wanachama wapya tukutane haraka katika chumba cha mikutano, nambari 9,” Bw Muturi akasema.

Spika Muturi ndiye huwa mwenyekiti wa kamati hiyo. Wanachama wengine ni pamoja na; Kiongozi wa wengi Bw Kimunya, Kiongozi wa wachache John Mbadi, kiranja wa wengi Emmanuel Wangwe na kiranja wa wachache Junet Mohamed.

Bila kuundwa kwa HBC, bunge la kitaifa haliwezi kuendesha shughuli zake. Kamati hii ndio huamua miswada na hoja za kupewa kipaumbele kila wiki.

Miongoni mwa ajenda ambazo wabunge wanatarajiwa kujadili ni; bajeti ya ziada, makadirio ya bajeti ya kitaifa ya mwaka wa 2022/2023, miswada ya kupunguzwa kwa bei ya mafuta, miongoni mwa shughuli nyingine zenye umuhimu kwa taifa.