[ad_1]
Shule zakandamiza wazazi kwa kuwatoza ada za ziada zisizofaa
Na FAITH NYAMAI
SHULE kadhaa zimeendelea kupuuza masharti ya Wizara ya Elimu kuhusu karo na kuongeza ada za ziada huku zikiwashurutisha wazazi kulipa bila kuchelewa.
Katika shule zilizoathiriwa, wazazi wametakiwa kulipa ada za ziada kama vile malipo ya masomo ya ziada, ada ya mafunzo maalum, ada ya mitihani ya kitaifa, malipo ya kuwapa motisha walimu na pesa za ziara.
Katika shule ambazo miundomsingi yake iliharibiwa na mioto, baadhi ya shule ziliwatoza wazazi kiasi cha hadi Sh9, 000 huku nyingine zikitoza Sh5, 000 kwa kila mtoto.
Wazazi waliozungumza na Taifa Leo walisema shule zilianzisha ada hizo mpya za malipo pasipo kujadiliana wala kuwahusisha.
Mwenyekiti wa Muungano wa Wazazi, Nicholas Maiyo alisema licha ya onyo kutoka kwa Wizara ya Elimu na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), baadhi ya shule zimeendelea kukaidi utaratibu wa Wizara kuhusu karo.
“Baadhi ya wazazi wameripoti kwetu kuwa baadhi ya shule zinatoza Sh4,800 kwa mitihani ya kitaifa huku nyingine zikitoza ada za ziada kama malipo ya mafunzo ya ziada, ada za kuwamotisha walimu, ada za kiwango cha juu mno kwa ukarabati wa shule zilizoteketezwa muhula uliopita na pesa za ziara za shule,” alisema Bw Maiyo.
Kulingana na Bw Maiyo, baadhi za shule zilizoripotiwa kwa muungano kwamba zinaitisha ada za ziada ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Kitale, Shule ya Upili ya Kathiiani Girls, Shule ya Upili ya Uthiru Girls miongoni mwa nyingine.
“Shule ya Uthiru inawataka wanafunzi kulipa Sh2, 500 kama ada ya mafunzo ya ziada kila muhula,” alisema Bw Maiyo.
[ad_2]
Source link