Connect with us

General News

Sijaanza kampeni za urais, Ruto sasa asema – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Sijaanza kampeni za urais, Ruto sasa asema – Taifa Leo

Sijaanza kampeni za urais, Ruto sasa asema

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Dkt William Ruto amekana madai kwamba ameanza kampeni za mapema za kusaka kura za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea na wanahabari Jumatatu katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi,  Dkt Ruto alisema ziara ambazo amekuwa akifanya maeneo mbalimbali nchini ni za kukagua miradi ya serikali na kupata hisia za wananchi kuhusu utendakazi wa serikali.

Naibu Rais alieleza kuwa licha ya kwamba amekuwa akivalia mavazi yasiyo rasmi katika ziara hizo, hakuna sheria inayomlazimu kutelekeza majukumu yake rasmi akiwa amevalia suti na tai.

“Sijaanza kampeni kwa sababu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijatangaza rasmi kipindi cha kampeni. Kile ambacho nyinyi huona nikifanya ni wajibu wangu kama Naibu Rais. Hii ni kuwatembelea wananchi, kusikiza maoni yao na changamoto zao na kukagua miradi ya maendeleo na kama vile barabara,” Dkt Ruto akaeleza.

Alisema hayo baada ya kuongoza mkutano wa Baraza Shirikishi kuhusu  Bajeti na Masuala ya Kiuchumi (IBEC), ambayo ilisusiwa na mawaziri wanne walioalikwa.

Wao ni Ukur Yatani (Fedha), James Macharia (Uchukuzi), Peter Munya (Kilimo) na George Magoha (Elimu). Ni waziri wa ugatuzi Charles Keter aliyefika katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na magavana tisa.

Dkt Ruto alisema suala la ushirikishwaji wa umma katika masuala ya serikali ni hitaji muhimu la kikatiba kwa wananchi ndio hufaidika na utendakazi wa serikali. Kwa hivyo, akasema, majibu, maoni na hisia zao ni muhimu.

“Mkiniona katika sehemu mbalimbali nchini, ni kwa sababu mimi ni Naibu Rais na miradi ya  serikali imetapakaa kote nchini na hua nataka kupata majibu kutoka kwa wananchi kuhusu miradi hiyo,” Dkt Ruto akaongeza.

Naibu Rais alisema ataanza kampeni rasmi baada ya IEBC kutangaza rasmi kipindi cha kampeni.

Kauli ya Dkt Ruto inajiri baada yake kukosolewa kwa kuzuru maeneo mbalimbali nchini akivumisha chama cha United Democratic Alliance (UDA) na ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.

Vile vile, juzi Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliwakashifu wagombeaji wa urais ambao wameanza kampeni za mapema akisema hiyo ni kinyume cha sheria.