Simanzi watu sita wakiangamia Murang’a baada ya moto kuteketeza nyumba yao
NA MWANGI MUIRURI
WIMBI la simanzi limetanda katika Kaunti ya Murang’a baada ya familia moja kupoteza watu sita ndani ya mkasa wa moto unaokisiwa kuanzishwa kimakusudi Jumapili alfajiri.
Ripoti za upelelezi zilionyesha kuwa mama na watoto wake watatu sambamba na wajukuu wawili walikumbana na mauti baada ya nyumba walimokuwa wamelala katika kijiji cha Nguthuru kilichoko eneobunge la Kandara kupigwa kiberiti.
“Ni kisa cha kuhuzunisha na tayari tumepata mshukiwa mmoja ambaye tunamzuilia katika Kituo cha polisi cha Kabati. Mshukiwa huyo ni dadake mama watoto aliyeaga dunia katika mkasa huo,” akasema mkuu wa polisi wa Kandara Bw Michael Mwaura.
Bw Mwaura alisema kuwa mkasa huo wa saa kumi alfajiri ulitokea huku nyumba ya waathiriwa ikiwa imefungwa kutoka nje, hali ambayo ililemaza juhudu za kuokolewa.
“Mshukiwa tuliye naye mbaroni alikuwa akiishi pamoja na walioaga dunia lakini mnamo Junamosi, akahamisha vitu vyake. Duru zetu za upelelezi zinaashiria kuwa alitoka katika makazi hayo akiwa na tetesi tele za ukorofi. Ametajwa sana na wenyeji kuwa mshukiwa mkuu na ndipo tukamtia mbaroni,” akasema.
Wakuu wa vitengo vya usalama wakiongozwa na Kamanda wa polisi wa Kaunti Bw Ali Nuno walifika katika boma hilo na kuahidi haki kwa waathiriwa.
“Huu ni mkasa mkubwa sana na sisi katika vitengo vya kiusalama tunauwajibikia kwa uzito mwingi sana. Tutahakikisha kisa hiki kimechunguzwa na wote waliohusika wawajibishwe mkondo wa sheria,” akasema Bw Nuno.
Mbunge wa Kandara Bi Alice Wahome alihuzunika akisema kwamba “tunataka jibu la haraka kutoka kwa serikali.”
Aliteta kuwa visa kama hivyo vingezimwa ikiwa serikali ingekuwa imemakinikia suala la kutangamana na wananchi na kutambua hatari zinazotokota.
“Mkasa kama huu ni wa kupangwa kwa muda. Hatari hii ikijiunda; swali linalosumbua ni walimokuwa wadau muhimu wa masuala ya kiusalama. Kuanzia naibu wa chifu, chifu na kamati zao za ujasusi. Wahusika wa Nyumba Kumi na pia mbona harakati za kuokoa zilikwama wapi moto huo ukivuma na kuua,” akahoji.
Seneta wa Murang’a Dkt Irungu Kang’ata alisema kuwa hadi sasa hakuna sababu za kuridhisha ambazo zimetolewa na vitengo vya kiusalama.
“Mazoea ya wakuu wa vitengo vya usalama kujitokeza katika mikasa ya uhalifu na kutusimulia jinsi ilivyofanyika na kwamba maiti zimepelekwa mochari huku uchunguzi ukiendelea ni sawa na kutukejeli. Vitengo hivyo vinafaa kumakinikia hatari za uhalifu na ujambazi kwa njia pana zaidi,” akasema Dkt Kang’ata.
Aliongeza kuwa viongozi wa kaunti watashirikiana katika kuomboleza na kuandaa maziko, huku akiwataka maafisa wa polisi wasake na watekeleze haki.
Miili ya wote ilipelekwa hadi mochari kuhifadhiwa huku ikingoja upasuaji wa kitaalamu kubaini hali yao kabla ya kukumbwa na mauti hayo.