Siri ya mawaziri ‘wanasiasa’ kutojiuzulu viti
BI TAIFA WANDERI KAMAU NA GITONGA MARETE
HATUA ya baadhi ya mawaziri kudinda kujiuzulu kutoka nafasi zao kuwania nyadhifa za kisiasa kwenye uchaguzi wa Agosti, imetajwa kuchangiwa na miegemeo ya kisiasa katika maeneo wanakotoka.
Wadadisi wa siasa wanasema kuna uwezekano pia baadhi yao wamebaki serikalini ili kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta kumaliza miradi yake na kumfanyia kampeni kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kupitia vuguvugu la Azimio la Umoja.
Baadhi ya mawaziri waliotarajiwa kujiuzulu lakini wakakosa kufanya hivyo ni Peter Munya (Kilimo), Mutahi Kagwe (Afya), Eugene Wamalwa (Ulinzi) na Ukur Yatani (Fedha).
Bw Munya alitarajiwa kujiuzulu ili kuwania ugavana katika Kaunti ya Meru, sawa na Bw Kagwe, aliyetajwa kumezea mate nafasi ya ugavana katika Kaunti ya Nyeri.
Ingawa haikubainika nafasi ambayo angewania, Bw Wamalwa alitarajiwa kuwania ugavana katika Kaunti ya Trans-Nzoia, ikizingatiwa anatoka eneo la Saboti.
Bw Balala alitarajiwa kuwania useneta au ugavana katika Kaunti ya Mombasa, ikizingatiwa aligombea useneta katika kaunti hiyo mnamo 2013 kwa chama cha Republican Council (RC), japo akashindwa na Bw Hassan Omar.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa Kipkorir Mutai, Rais Kenyatta angejipata mpweke kisiasa ikiwa mawaziri hao wangejiuzulu, hivyo kufanya vigumu kwake kusukuma mipango ya serikali katika hatua za mwisho za utawala wake.
“Ukiangalia kwa kina, mawaziri hao wote ni wanasiasa ambao washawahi kuhudumu katika nyadhifa tofauti za kisiasa awali.
Hivyo, hilo linawafanya kuwa nguzo kuu kwa Rais Kenyatta anapojitayarisha kuwaonyesha Wakenya mafanikio aliyopata katika utawala wake,” asema Bw Mutai.
Kwa mfano, anamtaja Bw Munya kuwa nguzo kuu kwenye uendeshaji wa mipango ya serikali katika sekta ya kilimo, ambayo Rais analenga kuilainisha kabla ya kung’atuka uongozini.
“Sekta ya kilimo ni kati ya zile ambazo Rais Kenyatta ametumia muda wake mwingi kuilainisha kutokana na matatizo yaliyokuwa yakiikabili. Mageuzi mengi kwenye sekta kama za majanichai, kahawa na sukari yalianzishwa na Bw Munya baada ya Rais kumfuta kazi Bw Mwangi Kiunjuri. Hivyo,
waziri huyo angeacha pengo kubwa katika wizara hiyo muhimu,” akasema Bw Mutai.
Vilevile, anamtaja Bw Munya kuwa nguzo kuu ya kisiasa kwenye juhudi za Rais Kenyatta kumfanyia kampeni Bw Odinga, hasa katika eneo la Mlima Kenya. Wadadisi wanasema huenda Bw Munya pia anatayarishwa kwa nafasi kuu ya siasa, kama vile mgombea-mwenza wa Bw Odinga.
“Bw Munya amekuwa akitajwa kuwa miongoni wa watu wenye uwezekano mkubwa kumrithi Rais Kenyatta kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya. Tangu kuteuliwa kama waziri, amejitokeza kuwa nguzo kuu kisiasa na kikazi,” asema Prof Macharia.
Prof Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa. Mdasisi huyo hata hivyo anasema uamuzi wao umeoanishwa na ahadi za kisiasa, ikiwa Bw Odinga ataibuka mshindi kwenye uchaguzi wa urais.
“Ni wazi Rais Kenyatta anamuunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wake. Ikiwa Bw Odinga ataibuka mshindi, watakuwa kwenye nafasi kubwa ya kuvuna kisiasa kwa kumsaidia Rais kuendesha ajenda zake. Uteuzi wao bila shaka utakuwa kama ‘malipo’ au zawadi kwao,” asema Prof Munene.
Vivyo hivyo, anasema hawatapoteza lolote kisiasa, ikiwa Bw Odinga hataibuka mshindi.
Next article
Vyama tayari kuvuna kupitia mchujo