Sitafuti kuwa naibu wa Raila – Kinyanjui
Na ERIC MATARA
GAVANA wa Nakuru Lee Kinyanjui amesema kuwa hana mpango wa kuwa mwaniaji mwenza wa kinara wa ODM Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022.
Badala yake, Bw Kinyanjui alisema kuwa atatetea kiti chake cha ugavana katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Gavana huyo aliyekuwa akizungumza katika eneo la Rongai alipokuwa akitoa hatimiliki za mashamba kwa Wakimbizi wa Ndani kwa Ndani (IDPs), sasa amemaliza minong’ono ambayo imekuwepo kwamba alikuwa na nia ya kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.
Tetesi hizo ziliibuka baada ya kuonekana akiandamana na Bw Odinga kwenye mikutano mbalimbali ya kampeni nchini.
Bw Odinga anatarajiwa kutangaza azma yake ya kuwania urais Desemba 9, 2021.
Alipokuwa akizungumza kwenye mahojiano na vituo vya redio vinavyotumia lugha ya Kikamba wiki iliyopita, Bw Odinga alisema kuwa hajateua mwaniaji mwenza kufikia sasa.
“Mimi sijatangaza kwamba nitawania urais. Vilevile, madai kwamba nitateua mwaniaji wangu kutoka eneo la Mlima Kenya si ya kweli – hakuna uamuzi ambao umefanywa,” akasema.
Bw Kinyanjui alishikilia kuwa atawania tena kwa muhula wa mwisho ili kumalizia miradi yake ya maendeleo aliyoianza katika muhula wa mwisho.
“Ninajua watu wananiombea niwe naibu rais. Si vibaya. Hiyo inaonyesha kuwa Wakenya wananiamini. Lakini nathibitisha kuwa nitawania ugavana wa Nakuru katika Uchaguzi Mkuu ujao,” akasema Bw Kinyanjui.
Bw Kinyanjui atamenyana na wanasiasa wanne ambao tayari wametangaza nia ya kuwania ugavana mwaka 2022.
Miongoni mwao ni hasimu wake wa kisiasa wa muda mrefu Seneta Susan Kihika wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu wa Rais William Ruto.
Bw Kinyanjui alifichua kuwa atatetea kiti kupitia chama chake cha Ubuntu People’s Forum (UPF).
“Mimi ni mwanachama wa Jubilee. Lakini sasa nimeungana na wanasiasa wenzangu wenye maono sawa na tumeunda chama cha UPF. Tutatumia chama hiki kutetea masilahi ya wakazi wa Nakuru ndani ya serikali ijayo,” akasema Bw Kinyanjui.
Alisema kuwa japo, UPF hakijazinduliwa rasmi, kimekuwa na uungwaji mkono mkubwa katika maeneo mbalimbali ya Kenya.
Awali, chama cha UPF kilikuwa kikijulikana kama Citizens Convention Party (CCP) kabla ya kubadilishwa jina.
UPF inaongozwa na wandani wa Bw Kinyanjui, akiwemo Bw Samuel Kinya Rukahu ambaye ni kiongozi wa chama.Wengi wa viongozi wa UPF ni washauri wa kisiasa wa Gavana Kinyanjui.
Viongozi wengine wa UPF ni Kenneth Kuria Mbaria ambaye ni kiongozi wa vijana, Bi Beatrice Nyawira Wambugu (mwenyekiti) na Bw Njoroge Gichuhi (Katibu Mkuu).
Bi Nyawira ni mshauri wa masuala ya kisiasa wa Gavana Kinyanjui.
“Nitaunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022. Chama chetu kipya kinaunga Bw Odinga,” akasema Bw Kinyanjui.