Connect with us

General News

Sonko anapanga kujifufua Pwani? – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Sonko anapanga kujifufua Pwani? – Taifa Leo

Sonko anapanga kujifufua Pwani?

NA VALENTINE OBARA

GAVANA wa zamani wa Kaunti ya Nairobi, Bw Mike Sonko, ameibua gumzo katika Kaunti ya Mombasa kuhusu mipango yake ya kisiasa.

Mwanasiasa huyo alididimia punde baada ya kutimuliwa mamlakani mwaka wa 2020 kwa madai ya uongozi mbaya wa jiji kuu la Kenya, lakini ameonekana kuanza kujifufua baada ya kuingia Mombasa kwa kishindo mwishoni mwa mwaka uliopita.

Ijapokuwa Bw Sonko kwa muda mrefu amekuwa kama mkazi Mombasa kutokana na baadhi ya biashara anazoaminika kuwa nazo katika maeneo ya Pwani, hatua yake ya kufungua kilabu cha burudani cha kifahari katika eneo la Shanzu umesababisha mdahalo mkubwa.

Hatua hiyo ingechukuliwa tu kama moja ya uwekezaji wake Pwani ambao hata umesababisha steji ya matatu maeneo ya Kisauni kubandikwa jina lake, lakini taarifa aliyotoa wiki iliyopita imechochea wadadisi wa kisiasa kushuku iwapo anataka kiti cha kisiasa, hasa ugavana katika kaunti hiyo au la.

“Katika siasa hakuna chochote kisichowezekana. Akipata fursa ya kuingia katika muungano wa kisiasa utakaokuwa na umaarufu Mombasa, bila shaka atajaribu bahati yake,” akasema mchanganuzi wa siasa, Bw Collins Ouma.

Bw Sonko amekuwa akidaiwa mara kwa mara kwamba angependa kuwania ugavana sehemu nyingine nje ya Nairobi lakini hajajitokeza wazi kuthibitisha hilo.

Katika taarifa yake, alidokeza kuhusu uwezekano wake kuwania wadhifa katika uchaguzi ujao ingawa hakufichua mengi kuhusu mpango wake.

Huku akiahidi “tetemeko la ardhi” kisiasa hivi karibuni, alisema muda bado.

Alidai kuwa hivi sasa wanasiasa ambao si maarufu ndio wametimua mbio kujipigia debe kabla siku rasmi ya kampeni za uchaguzi ujao kufika.

Alithibitisha kuna watu wanao-muuliza kila mara kama atawania kiti chochote katika uchaguzi ujao lakini akasema biashara anazoendelea kufungua zimenuiwa kumpa rasilimali za kuendelea kusaidia jamii jinsi alivyokuwa akifanya tangu zamani, na pia kutoa nafasi za ajira.

Shughuli zake za kutoa misaada zilipata pigo baada ya mahakama kuamuru baadhi ya akaunti zake za benki zifungwe, katika kesi inayohusu madai kwamba alishiriki njama za kuhalalisha pesa ambazo zilipatkana kwa njia haramu.

“Mimi na kikosi changu tumeamua kuanzisha biashara katika Kaunti za Mombasa, Nairobi, Kilifi, Kwale na Machakos tukiwa katika safari ya kufungua sehemu za burudani. Kilabu cha Volume VIP kilicho Shanzu, Kaunti ya Mombasa, ni chetu cha kwanza,” akaeleza.

Hata hivyo Bw Ouma alizidi kusema itabidi mbunge huyo wa zamani wa Makadara atangaze mwelekeo wake mapema kwani akiamua kuwania ugavana Mombasa, atasimama dhidi ya wanasiasa ambao tayari wana uzoefu mkubwa wa eneo hilo.

Mapema wiki hii, kilabu hicho kiligonga vichwa vya habari ilipodaiwa kuwa mwanamume alitiliwa dawa za kumpumbaza na mwanamke ambaye walikuwa wamekutana naye hapo, akaibiwa takriban Sh600,000.

Bw Sonko alipuuzilia mbali madai hayo yaliyosambazwa kupitia taarifa ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), na kusema ni njama za kuharibia sifa biashara zake kwani kisa hicho hakikifanyika katika kilabu chake.