[ad_1]
Staa wa Bandari FC Shaaban Kenga kurudi uwanjani
NA ABDULRAHMAN SHERIFF
BAADA ya kukosa kuichezea timu yake ya Bandari FC kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, Shaaban Kenga amewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa majuma machache yajayo atakuwa uwanjani kujumuika na wenzake kuifanikisha.
Akiongea na Taifa Leo siku moja baada ya kutolewa vyuma alivyowekwa kwenye mguu wa kushoto uliovunjika, Kenga alisema kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili alikuwa akifanya mazoezi kabla ya kutolewa kwa vyuma hivyo.
“Hivi sasa ninatarajia kupumzika kwa kipindi cha mwezi mmoja kuuguza jeraha la kutolewa vyuma na nikipona tu, nitarudi uwanjani kupigania namba ili tuweze kuisaidia timu yetu kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu ya FKF-PL na mashindano mengine,” alisema mwanasoka huyo.
Kenga ambaye alikuwa nahodha wa Bandari kabla ya kuvunjika mguu, anasema amekuwa na subira kipindi hicho cha mwaka mmoja na nusu na anawashukuru mashabiki wake waliokuwa mara kwa mara wakimpa moyo kuwa iko siku atarudi tena kiwanjani.
“Ninaamini sijapoteza kipaji changu kwani nilipofanya mazoezi nilijiona kuwa nitaweza kurudia mchezo wangu. Nawahakikishia wapenzi wa Bandari kuwa niko njiani kurudi kuichezea timu ambayo nimeipenda kidhati,” akasema.
Kenga ambaye ni mchezaji mkongwe zaidi wa timu hiyo aliyojiunga tangu mwaka 2011 anasema anafurahikia jinsi timu hiyo inavyojitahidi na kuthibitisha kuwa miongoni mwa zile zenye matumaini ya kushinda taji la ligi hiyo kwani timu za juu zimepishana na pointi kidogo.
“Nina matarajio makubwa ya kujiunga na wenzangu baada ya mwezi mmoja kwani sasa ninajituliza ili nipone vidonda kwa haraka. Mpira ni mchezo ulioko moyoni mwangu na ninapenda nichezee Bandari hadi nitakapostaafu,” akasema.
Kenga alianza soka kwa kuchezea klabu ya Mariakani FC kabla ya kujiunga na Gunners FC ya Magongo mjini Mombasa ambako maskauti wa Bandari walimshuhudia na akasajiliwa.
Next article
Natembeya ajitunuka sifa akisimulia jinsi alivyokabili…
[ad_2]
Source link