Tabasamu tele ufuo wa Pirates ukifunguliwa upya kwa umma
Na WINNIE ATIENO
SERIKALI ya kitaifa na ya Kaunti ya Mombasa, hatimaye zimefungulia umma ufuo wa bahari wa Jomo Kenyatta.
Wafanyabiashara walikuwa wamezuiwa kuingia katika ufuo huo ulio maarufu kama ‘Pirates’ kwa miaka miwili iliyopita ili kutoa nafasi ya ukarabati wa Sh200 milioni.Kwa upande mwingine, wananchi walizuiwa kuutumia kwa sababu ya juhudi za kuzuia ueneaji wa virusi vya corona kupitia kwa mtagusano.
Mwenyekiti wa wahudumu wa ufuoni, Bw Paul Munza, alisema wana matumaini ya kufaidika kwani kanuni nyingi za Covid-19 sasa zimetolewa baada ya maambukizi kupungua, na pia msimu mkuu wa utalii umekaribia.
“Tunaelekea katika msimu mkuu wa utalii ambapo maelfu ya watalii kutoka maeneo ya bara hufurika Pwani kwa shamrashamra za Desemba,” akasema Bw Munza.Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, ambaye alikuwa amewasilisha hoja bungeni kutaka serikali ishurutishwe kufungua ufuo huo,
alitoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kufuata kanuni zote za kuepusha ueneaji wa virusi vya corona.Vilevile, aliwataka wawe na nidhamu ya hali ya juu ndipo wavutie wateja kwa biashara zao huku akiwashauri wapokee chanjo ya kuepusha ugonjwa wa virusi vya corona ili watalii wasiwe na hofu wanapotafuta huduma zao.
“Lazima muwe na nidhamu, la sivyo, mtapoteza wateja ambao ni watalii. Lazima pia mfuate masharti yanayohusu Covid-19 ikiwemo kuosha mikono, kutumia vieuzi, kuepusha mtagusano na kuvaa barakoa. Bado hatari ipo.
Lazima tuwe na uwezo wa kuvutia watalii wa kigeni,” akasema, alipokutana na wafanyabiashara hao Jumamosi.Kwa kipindi ambapo ufuo huo wa Pirates ulifungwa, ilibainika kuwa watu wachache wenye uwezo wa kukodisha huduma kama vile kuendeshwa kwa boti, ndio waliokuwa wakiruhusiwa kuingia kwa njia za magendo.
Baadhi ya wakazi wakati huo walilalamika kuwa hali hiyo ilibagua wengi wasio na uwezo wa kifedha ambao kwa kawaida hutegemea kuvinjari katika ufuo huo wa umma. Miezi miwili iliyopita, Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, aliagiza maafisa wa Kaunti kutafuta jinsi wafanyabiashara hao wanaozidi 400 wangeruhusiwa kurudia biashara zao katika ufuo huo.
Ufuo wa Pirates ndio mkubwa zaidi wa umma eneo la Pwani ambao huvutia maelfu ya watalii wa nchini na kimataifa.Ukarabati ambao sasa umelengwa kuanza Februari mwaka ujao umelenga kuufanya ufuo huo kufikia hadhi ya kimataifa ili kuimarisha utalii Mombasa.
Next article
Waziri asema wauguzi hawakufeli mtihani