NI miaka minne sasa tangia aanze kushiriki masuala ya uigizaji anakoamini ipo siku atawika na kuibuka kati ya kina dada wanaotawala katika tansia ya maigizo barani Afrika.
Nicole Awinja Amimo ni mwigizaji anayekuja huku akilenga kutinga upeo wa kimataifa katika maigizo. Kando na uigizaji dada huyu ni mfanyi biashara, mpodoaji (makeup artist), muimbaji, mshauri wa masuala ya fedha pia msomi wa mwaka wa nne kwenye Chuo cha Multimedia (MMU) anakosomea kuhitimu kuwa mwana habari.
”Ninaamini ninatosha mboga kufanya kweli katika uigizaji miaka ijayo,” anasema na kuongeza kuwa anafahamu sio mteremko kukwea mlima huo. Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1997 ingawa anasema alivutiwa na masuala ya uigizaji tangia akiwa mtoto zaidi alipata motisha baada ya kutazama filamu za msanii Sanaipei Tande maarufu kama Sana. ”
Ninadhani pia nilipata msukumo wa damu katika familia yetu maana mjomba wangu ni mwigizaji,” akasema na kuongeza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo analenga kuwa kati ya waigizaji mahiri hapa nchini.
Dada huyu amefanikiwa kushiriki filamu tatu ikiwamo ‘The stringed’ (KBC) na ‘Date my family’ (Maisha Magic Plus). Katika mpango mzima kisura huyu anasema kwenye uigizaji analenga kufuata nyayo za Mkenya mwenzake, Lupita Nyong’o anayetamba katika filamu za Hollywood.
Kwenye juhudi za kujikuza anasema anatamani sana kuchapa shughuli na waigizaji wanaotamba barani Afrika akiwamo Mercy Johnson mzawa wa Nigeria aliyeshiriki filamu kama “The Maid,’ ‘Hustlers,’ na ‘A Naija Christmas’ kati ya zingine.
Pia Tonto Dikeh (Nigeria) aliye pia muimbaji aliyeshiriki filamu kama ‘Men in love,’ ‘Stolen kiss,’ na ‘Dirty Secret.’ Kwa humu anasema angefurahi kujikuta jukwaa moja na wenzake akiwamo Sarah Hassan na Sanaipei Tande.
CHANGAMOTO
Anasema uigizaji unahitaji muda mwingi ambapo nyakati nyingi wasanii hukosa muda kuwa na wana familia. ”Nyakati zingine wasanii hufanya kazi na kutolipwa ambapo hali hiyo hutuvunja moyo vibaya,” akasema. Tatizo lingine anasema wapo maprodusa wengi tu hupenda kushusha hadhi ya mwanamke ambapo huwataka kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi ili wapate ajira.
USHAURI
Anashauri wasanii wanaoibukia kuwa ili kutimiza malengo yao itawabidi wajikaze pia wajitume kiume bila kulaza damu kwenye masuala ya uigizaji. ”Hakuna chochote huja rahisi bali lazima tukifanyie kazi ndivyo ninavyoweza kuwaambia wasanii wenzangu,” akasema na kuwaomba kamwe kutoruhusu team mafisi kuvuruga mipango zao.
Anasema serikali inapaswa kusaidia sekta ya uigizaji kwa njia tofauti ikiwamo kupiga jeki kifedha ili kugharamia shughuli za production. Pia kuandaa tuzo kwa mfano filamu bora katika kategoria tofauti, waigizaji nora kitengo cha wanaume na wanawake ili kuwapa motisha watie bidii wanapopiga shughuli. Anatoa mwito serikali ianzishe mikakati mwafaka itakayofungua mwanya mzuri ili waigizaji chipukizi nchini kunoa`talanta zao.