Teknolojia kusaidia wakulima kupunguza hasara mashambani
NA RICHARD MAOSI
Kukausha matunda ni njia mojawapo ya kuyahifadhi ili yaweze kutumika kwa muda mrefu, baada ya kuyavuna kutoka shambani.
Mfumo huu wa kuyakausha, unahusisha kuondoa chembechembe za maji ndani ya matunda. Mbinu hii iwapo itazingatiwa na wakulima wengi, itasaidia kuwaepushia hasara hasa msimu wa mavuno ambapo baadhi ya mazao hushuhudia kiasi kikubwa cha mazao na kuchangia baadhi kupata hasara kwa sababu matunda mengi huwa yanaharibika upesi.
Pia tatizo la uchukuzi huchangia mazao mengi ya shambani kuharibika.“Matunda yaliyoivia shambani yanaweza kuharibika, na hiyo kusababisha hasara kubwa kwa sababu hayawezi kufika sokoni kwa wakati ambao unafaa, labda kutokana na miundo misingi duni,” anasema Pauline Okubasu kutoka eneo la Kyumbi, Kaunti ya Machakos.
Pauline anafanya kazi ya kuandaa matunda yaliyokaushwa na hatimaye kuwauzia wateja kutoka Nairobi, Machakos, Malindi na Nakuru.
Hii ikitokana na ushirikiano mkubwa anaopata kutoka kwa wakulima wa matunda hususan wa maembe na machungwa kutoka kaunti ya Kitui, Makueni, Voi na Machakos.
Mwaka wa 2020, kulipozuka janga la Covid 19, wakulima wengi walikuwa wakipata changamoto kwa ukosefu wa namna ya kusafirisha mazao yao hadi sokoni, ndiposa akapata wazo la kuwasaidia.
Anasema hii ni kutokana na vizuizi vingi vya usafiri ambavyo vilifanya baadhi ya wakulima kukata tamaa na kuachana na shughuli za ukulima wa matunda na kugeukia aina nyingine ya kilimo.
“Kwa kutumia aina maalum ya mtambo unaofahamika kama drier (kifaa cha kukausha) huwa naweza kukausha ndizi, mananasi na maembe kisha kuyapakia kwa ajili ya wanunuzi wangu, wengi ambao wanatoka nje ya Kaunti ya Machakos,” anaeleza.
Aidha Pauline anaamini kuwa mtambo wa kukausha matunda utasaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwa kuhifadhi matunda kwa muda mrefu bila kuharibika.
Hii ni kwa sababu inakisiwa kuwa takriban asilimia 40 ya matunda huharibika yakiwa yangali shambani kwa sababu ya ukosefu wa soko na hiki ni chakula ambacho kinaweza kutumika kuwalisha raia wanaopatikana katika maeneo ambayo yana uhaba.
Mtambo wake wa kukausha matunda, una uwezo wa kuchukuamuda wa saa nane tu kukausha matunda, ambayo hatimaye yanaweza kudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Ni kifaa ambacho kinafanana na jokofu, hutumia umeme, lina eneo ambapo moto huwekwa ili kutoa mvuke wenye joto ambao ndio hukausha matunda na kuyaacha yakiwa kavu, pamoja na feni ambayo hutumika kusawazisha kiwango cha joto ndani ya mtambo huo wa kukausha matunda.
“Wakulima wengi wa maembe kutoka eneo hili, kwa muda walikuwa wakitupa maembe mengi kwa sababu ya ukosefu wa nyenzo mwafaka za kutunza matunda yao ambayo mara nyingi huchukua siku mbili tu kabla ya kuharibika,’akasema.
Anasema kuwa kutokana na mtambo huu, anaweza kukausha takriban kilo 500 ya maembe kwa siku moja hata wakati ambapo mvua ni nyingi na wala hakuna jua.
Matunda yaliyokaushwa huuzwa msimu wa kiangazi na soko lake ni zaidi ya mara tano kiwango cha mazao ghafi kutoka shambani, ambayo huuzwa kwa bei ya chini.
Wanunuzi wake wengi wakiwa ni wakazi wa mji wa Nairobi na wasafiri wanaotumia barabara ya Nairobi ukielekea Mombasa, ambapo gramu 100 ya maembe yaliyokaushwa huuzwa kwa Sh100.
Kulingana na Pauline ana matumaini makubwa kwa ajili ya siku zijazo ambapo anaamini kuwa wakulima wengi zaidi watajipatia mtambo huu ili uwasaidie kupunguza hasara wanayopata hususan mazao yao yanapokosa kufika sokoni kwa wakati unaofaa.
“Maeneo mengi ya Ukambani hushuhudia kiwango kidogo cha mvua hivyo basi wakulima wengi hutegemea matunda ambayo mara nyingi huja kwa msimu baina ya Agosti na Februari kila mwaka.”
Isitoshe anaamini kuwa ukaushaji wa matunda utasaidia kukuza sekta ya viwanda na biashara na pia kuzingatia uhifadhi wa virutubishi vya asilia ambavyo ni muhimu kwa afya ya binadamu, mbali na kubuni nafasi nyingi za ajira kwa vijana.
Next article
Mpango wa Ajira Digital kuwezesha vijana kubuni njia za…