Connect with us

General News

Teknolojia ya mHealth yapigisha hatua utoaji wa huduma za kiafya – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Teknolojia ya mHealth yapigisha hatua utoaji wa huduma za kiafya – Taifa Leo

MAKALA MAALUM: Teknolojia ya mHealth yapigisha hatua utoaji wa huduma za kiafya

NA WINNIE ONYANDO

ALICE Nyakundi, 50, ni daktari katika kituo kimoja cha afya jijini Nairobi na amekuwa akitumia programu ya kidijitali ya Smart Patient App kufuatilia hali ya mgonjwa anayeishi Kaunti ya Kisumu na ambaye anakabiliwa na shinikizo la damu.

Anasema kuwa mgonjwa wake amefaidika sana kutokana na programu hiyo ya kidijitali hasa baada ya kuhamishwa kutoka hospitali moja Kisumu na kuletwa kuhudumu jijini Nairobi.

“Ni miaka miwili sasa tukiwasiliana na mgonjwa wangu. Kupitia programu hiyo, napata kujua ikiwa anapata nafuu au la. Kadhalika, naweza kumpendekezea tiba,” akasema Dkt Nyakundi.

Kulingana na Ruwaza 2030 ya sekta ya Afya, Mkurugenzi wa Utoaji Huduma za Kimatibabu, Kioko Jackson, alisema utoaji huduma za kimatibabu kupitia njia za kidijitali itasaidia pakubwa katika kutimiza maono hayo.

“Kenya inalenga kutoa huduma bora, kwa gharama ya chini na kwa kila mtu katika Ruwaza yake ya 2030. Ikiwa tutaendelea kutumia programu za kidijitali, basi tutaweza kutimiza hata kabla ya mwaka huo kufika,” akasema Dkt Kioko katika taarifa.

Katika miaka ya hivi karibuni, matumizi ya programu za kidijitali almarufu mHealth imeongozeka.

Hii ni kwa sababu ya upenyezaji wa hali ya juu wa rununu na ufikiaji wa mtandao, kwa hivyo, mHealth ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati ya kuzingatiwa katika utekelezaji wa Mkakati wa Afya wa nchi wa 2016-2020.

Mfumo wa afya nchini unaendelea kuimarika huku baadhi ya kaunti 47 zikikumbatia utoaji huduma za kimatibabu kidijitali.

Kitengo cha mHealth, kwa kushirikiana na Chama cha Taarifa za Afya nchini (KeHIA), pia kinaongoza katika utekelezaji wa miradi mipya ya kitaifa kama vile uundaji wa programu ya kuhifadhi maelezo ya kibinafsi ya mgonjwa, taarifa kamili kuhusu aina ya ugonjwa anayougua mhusika na kuanzisha mfumo wa uidhinishaji wa Mifumo ya Taarifa za Afya (HIS).

Baadhi ya idara za afya ambazo zimekumbatia mfumo wa kidijitali ni Idara ya Kutathmini Kiwango cha Ugonjwa (CCC) ambayo inatumia kompyuta kwa asilimia 88 kutoa huduma.

Kadhalika, Idara ya malipo inatumia mfumo wa kidijitali kwa asilimia 26. Hata hivyo, kuna haja kwa hospitali au vituo vya afya kukumbatia mfumo wa kidijitali hasa katika kufuatilia hali ya wagonjwa waliolazwa.

Huduma zinazotolewa kupitia programu hizo ni upendekezaji wa tiba na ushirikiano na mawasiliano ya karibu kati ya mgonjwa na daktari wake.

Kadiri simu za rununu na programu mbalimbali za kutolea huduma za kimatibabu zinavyozinduliwa, wengi sasa wameanza kuchangamkia huduma za kimatibabu kidijitali.

Lengo la jumla la viwango vya mHealth nchini Kenya ni kuhakikisha muundo, maendeleo na utekelezaji wa masuluhisho ya mHealth yanayoshirikiana, yanayoweza kupanuka na endelevu ambayo yanawanufaisha wateja na wahudumu wa afya kwa njia ya umoja na ya kiujumla kwa matokeo bora ya afya.

Anaposajiliwa katika programu husika ya kidijitali, baadhi ya maelezo muhimu yanayofaa kujumuishwa ni majina, namabari ya simu, umri, jinsia, miaka, anakoishi na jina la kituo cha afya husika.

Kama njia ya kuimarisha sekta ya utoaji wa huduma za kimatibabu kidijitali, Shirikisho la wahudumu wa afya nchini (KMA) liliweza kusaini mkataba wa kushirikiana na shirika la Smart Applications International.

Alipohojiwa na Taifa Leo jijini Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Smart Applications International, Harrison Muiru alisema kuwa ushirikiano huo utasaidia kuendeleza ukuaji wa matibabu wa kidijitali na hata kuwapunguzia wagojwa mzigo wa kusafiri kutafuta matibabu.

Alisema pia ushirikiano huo unalenga kuhamasisha umma kuhusu matibabu kupitia mfumo wa kidijitali.

“Kwa sasa, asilimia 30 ya Wakenya wanatumia programu mbalimbali za kidijitali ili kupata huduma za kimatibabu. Ushirikiano wetu na KMA utasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa hospitalini. Tunataka kila mmoja akumbatie matibabu ya kidijitali,” akasema Bw Muiru.

Kwa upande wake, rais wa KMA, Were Onyino, alisema wananuia kutumia programu kama vile Smart Patient Engagement App na SmartHealth+ ili kuendeleza utoaji wa huduma za kimatibabu kidijitali.

“Kupitia programu hizo mbili, itakuwa rahisi wagonjwa kuzungumza na madaktari wao. Kadhalika, madaktari pia wataweza kuweka rekodi zao kwa njia za kidijitali ili kupunguza mrundiko wa faili ofisini,” akasema Dkt Onyino.

Jinsi mgonjwa anavyoweza kulinda maelezo yake ya kibinafsi katika programu za mHealth

Mtaalamu wa masuala ya usalama mtandaoni, Maria Garnaeva wa kampuni ya Kaspersky anapendekeza njia za kulinda maelezo ya kibinafsi mtandaoni ambazo zinajumuisha utumiaji wa nenosiri thabiti au hata kuweka nenosiri mara mbili ili mtu asiweze kuingia katika programu inayobeba maelezo yake ya afya.

Kadhalika, anaweza kutumia nenosiri ambalo si rahisi mtu kuiba ama kugundua.

Mgonjwa au anayetumia programu za kidijitali za afya anafaa kuweka programu maalum ambayo ina uwezo wa kufuta kabisa au kuficha maelezo yake ya afya endapo simu yake itaibiwa.

Mtumiaji wa programu hizo pia anafaa azime au kuepuka kupakua programu ambazo zinamwezesha yeye kumtumia mwingine data ama maelezo kutoka kwa simu yake ya mkono.

Kadhalika, mtu anafaa atumie programu thabiti ambazo zinawazuia watu wasiofaa kuingia kwenye simu yake na kusoma melezo yake.

Anayetumia mHealth pia anafaa kuweka programu ya usalama ili kulinda melezo yake dhidi ya programu hasidi, virusi, vidadisi na mashambulizi yanayotokana na programu hasidi. Watumizi pia wanafaa kutafiti juu ya programu za simu kabla ya kuzipakua.

Tunza simu yako vizuri. Hakikisha kuwa unaibeba mwenyewe kila wakati ili kupunguza hatari ya matumizi yasiyoidhinishwa.

Dumisha usalama wa kutosha wakati unatuma au kupokea taarifa za afya kupitia mitandao.

Futa taarifa zote za afya zilizohifadhiwa kwenye simu yako kabla ya kumpa mtu au kuacha kuitumia.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending