Tuambiwe ukweli, nani huchoma soko la Gikomba? Wakenya Twitter wawaka
Na WANGU KANURI
WAKENYA katika mtando wa kijamii wa Twitter wameghadhabishwa na visa vya moto vinavyozuka kila mara katika soko la Gikomba, Nairobi.
Kisa cha hivi punde kilichofanyika Jumatatu asubuhi, kinajiri baada ya Idara ya Huduma za Jiji (NMS) kusema kuwa wamepokea notisi ya kuwafukuza wauzaji 174 wa Gikomba ili ujenzi wa hospitali ya Pumwani Majengo upanuke.
Japo chanzo cha moto huo hakijaelezwa, Wakenya hawajaridhishwa huku wauzaji wakikadiria hasara kubwa.
“Soko la Gikomba linateketea saa chache baada ya korti kuidhinisha NMS kuwafukuza baadhi ya wauzaji. Sasa tuelezeni ni nani huchoma soko la Gikomba?” akauliza Wambo.
“Ikiwa serikali haijaweza kuwashika wanaocteketeza soko la Gikomba hadi wa leo, basi watawezaje kujua sababu kuu ya mioto za shule za upili? Tayari mabweni yamechomwa na badala ya kujiuliza kwa nini wameanza kutathmini adhabu shuleni,” akasema Bravin Yuri.
“Soko la Gikomba limejengwa kwa shamba la nani? Labda hiyo ndiyo sehemu ya fumbo. Labda hiyo ndiyo suluhu pekee la kumaliza mioto hii inayozuka kila mara ni kwa kuwa na mijengo maalum ya wauzaji. Ama mijengo hiyo itachomwa kama mabweni shuleni?” akauliza Dkt John Njenga.
“Kuchoma soko la Gikomba ni ishara ya kukosa utu. Watu wengi wataumia. Poleni watu wa Gikomba,” akasema Edwin Wafula.
“Soko la Gikomba limechomwa tena! Ni nani huanzisha mioto hii. Hata siku tatu hazijaisha tangu moto mwingine kuzuka,” akaandika Jane Irungu.
“Mbona kila mara soko la Gikomba? Tupo salama mikononi mwa nani? Inauma,” akasema Stephen Mukangai.
“NMS kupata notisi ya kuwafukuza wauzaji wa soko la Gikomba kisha soko hilo linateketea siku inayofuata! Hapo hakuna sadfa hapo. Tunajua ni nani anayechoma soko hilo sasa!” akaandika Charles Kabaiku.
“Sasa mmejua wanaokuwa wakiteketeza soko la Gikomba. Magaidi wa uchumi,” akasema Thuo Githuku.
Mwezi jana, moto mwingine ulizuka kusini mwa soko hilo katika sehemu ya Jua Kali karibu na Shule ya Msingi ya Muthurwa.
Mnamo Agosti mwaka huu, wauzaji walio na maduka karibu na eneo la Molo Line linalojulikana kama Ghorofani-Gikomba walikadiria hasara baada ya moto kuzuka na kuharibu mali yao.
Hata hivyo, fumbo la mwanzilishi wa mioto hiyo bado halina jibu.