[ad_1]
Tundo na Chager nje ya Kajiado Rally, macho kwa Karan Patel
Na GEOFFREY ANENE
BINGWA wa Afrika na Kenya 2021 Carl ‘Flash’ Tundo na mshindi wa zamani wa kitaifa Baldev ‘Boldy’ Chager ni majina makubwa yatakayokosa duru ya kufungua msimu 2022 ya Mbio za Magari za Kitaifa Kenya itakayoandaliwa eneo la Ilbissil, Kajiado hapo Januari 30.
Madereva 12 waliojiandikisha kushiriki ni pamoja na mshindi wa duru ya Voi Rally 2021 Karan Patel na bingwa wa Afrika kitengo cha chipukizi McRae Kimathi.
Patel atashirikiana na Tauseef Khana katika gari la Ford Fiesta. Kimathi, ambaye anajiandaa kuelekea nchini Norway kwa mafunzo ya mbio za magari kabla ya kushiriki duru sita za dunia, ataelekezwa na Mwangi Kioni katika gari la Subaru Impreza.
Madereva wengine waliothibitisha kushiriki ni Jasmeet Chana, Issa Amwari, Steve Mwangi, Nikhil Sachania, Daren Miranda, Kush Patel, Rajveer Thethy, Zameer Verje, Leo Varese na Sameer Nanji.
Tundo na Chager walidokeza mwisho wa msimu uliopita kuwa huenda wakashiriki duru chache msimu huu ama kustaafu.
Karan alishinda duru ya mbio zozote za magari mwezi Agosti mwaka jana mjini Voi baada ya mashindano 40 bila ushindi tangu aanze kushiriki fani hii mwaka 2014. Yeye ni mmoja wa wanaopigiwa upatu kufanya vyema Jumapili.
[ad_2]
Source link