AFCON: Tunisia wadengua Nigeria katika hatua ya 16-bora
Na MASHIRIKA
TUNISIA walitinga robo-fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mwaka huu baada ya kudengua Nigeria kwenye hatua ya 16-bora mnamo Jumapili usiku nchini Cameroon.
Bao la pekee katika mchuano huo lilifumwa wavuni na nahodha Youssef Msakni aliyemzidi maarifa kipa Maduka Okoye mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Kibarua cha Nigeria kurejea mchezoni baada ya goli hilo liligeuka kuwa mtihani mgumu baada ya fowadi wao Alex Iwobi kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea Msakni visivyo dakika chache baada ya kuletwa uwanjani katika kipindi cha pili.
Nigeria walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kukomoa Tunisia kirahisi ikizingatiwa kwamba ndicho kikosi cha pekee kilichofuzu kwa hatua ya 16-bora baada ya kushinda mechi zote za raundi ya makundi.
Nigeria walipoteza nafasi nyingi za kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia wavamizi Umar Sadiq na Moses Simon waliomshughulisha vilivyo kipa Bechir Ben Said.
Tunisia ambao walitwaa taji la AFCON mnamo 2004 walipokuwa wenyeji sasa watavaana na Burkina Faso katika hatua ya robo-fainali mnamo Jumamosi ya Januari 29, 2022.
Nigeria na Tunisia walikuwa wakikutana kwa mara pili chini ya kipindi cha miaka mitatu. Super Eagles ya Nigeria ilitandika Tunisia 1-0 katika mechi ya kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu kwenye makala yaliyopita ya AFCON nchini Misri mnamo 2019.
Kwa hivyo, Tunisia walijibwaga ulingoni wakiwa na kiu ya kulipiza kisasi japo waliambulia sare ya 1-1 mara ya mwisho walipovaana na Nigeria kirafiki mnamo Oktoba 13, 2020 ugani Jacques Lemans Arena, Austria.
Chini ya kocha mshikilizi Augustine Eguavoen, Nigeria sasa wanajiandaa kuvaana na Ghana katika michuano ya mikondo miwili ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.
Nigeria ni miongoni mwa vikosi vilivyokuwa vikipigiwa upatu wa kutia kapuni taji la AFCON mwaka huu ikizingatiwa ubora wa matokeo yao katika hatua ya makundi. Walifungua kampeni zao za Kundi D mwaka huu kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Misri mnamo Januari 11, 2022. Walipepeta Sudan 3-1 siku nne baadaye kisha wakalaza Guinea-Bissau 2-0 katika mchuano wa mwisho wa makundi ugani Roumde Adjia.
Matokeo hayo yaliwaweka kileleni mwa Kundi D kwa alama tatu zaidi kuliko Misri walioambulia nafasi ya pili baada ya kupiga Guinea-Bissau 1-0 na kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Sudan. Misri ambao ni mabingwa mara saba wa AFCON sasa watachuana na Ivory Coast katika hatua ya 16-bora.
Nigeria walitawazwa wafalme wa bara la Afrika mara ya mwisho mnamo 2013 baada ya kucharaza Misri 1-0 kwenye fainali nchini Afrika Kusini. Awali, walikuwa wametwaa ubingwa wa AFCON mnamo 1980 na 1994.
Tunisia walifuzu kwa hatua ya 16-bora wakiwa miongoni mwa vikosi viwili vilivyosajili matokeo ya kuridhisha katika raundi ya makundi ila vikaambulia nafasi ya tatu. Timu nyingine ni Comoros iliyokuwa katika Kundi C pamoja na Morocco, Gabon na wafalme mara nne, Ghana.
Tunisia walianza kampeni za Kundi F mwaka huu kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Mali mnamo Januari 12 ugani Limbe Omnisport. Waliponda Mauritania 4-0 katika mechi ya pili kabla ya limbukeni Gambia kuwaduwaza kwa 1-0. Gambia wanaonogesha fainali za AFCON kwa mara ya kwanza katika historia, sasa wataonana na Guinea katika raundi ya muondoano mnamo Januari 24, 2022.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO