MABINGWA wa Kenya, Tusker watakuwa mawindoni kufuta kichapo cha goli moja walichopokea kutoka kwa miamba wa Misri, Zamalek watakaporudiana katika mechi ya Klabu Bingwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ugani Borg El Arab mjini Alexandria mnamo Oktoba 22.
Vijana wa kocha Robert Matano wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusalia mashindanoni.
Mabingwa hao wa Kenya wa mataji 12 waliwasili nchini Misri Oktoba jioni baada ya kuondoka jijini Nairobi siku hiyo asubuhi.
Walipata kufanya mazoezi yao ya kwanza Jumanne usiku chini ya taa katika uwanja wa kupasha misuli moto nje ya ule wa Borg El Arab.
Tusker, ambayo inarejea kwenye mashindano haya ya haiba ya Afrika tangu msimu wa 2016-2017 ilipobanduliwa katika raundi ya kwanza, itategemea washambuliaji Boniface Muchiri na Mtanzania Ibrahim Joshua, kipa Brian Bwire na uongozi wa nahodha Eugene Asike.
Wanamvinyo wa Tusker wana kumbukumbu mbaya ugani Borg El Arab. Ni katikati uwanja huu walipochabangwa 2-0 na Wamisri Al Ahly na kubanduliwa kwenye kipute hiki kwa jumla ya mabao 4-1 katika raundi ya pili mwaka 2013 na pia kulimwa 3-0 na Al Ahly tena wakiaga mashindano kwa jumla ya mabao 5-0 katika raundi ya kwanza mwaka 2006.
Tusker FC yawasili katika uwanja wa ndege nchini Misri mnamo Oktoba 19, 2021. Picha/ Hisani
Vilevile, Tusker imepoteza michuano mitatu imewahi kucheza dhidi ya Zamalek tangu 2005 kwa hivyo ina kibarua kigumu cha kuingia awamu ijayo ya mechi za makundi.
Isipopata ushindi unaohitajika, Tusker itateremka katika mashindano ya daraja ya pili ya Afrika ambayo ni Kombe la Mashirikisho. Haitaingia moja kwa moja katika mechi za makundi ya kombe hilo. Vijana wa Matano watakutana na mmoja wa washindi 16 kutoka raundi ya pili ya Kombe la Mashirikisho ili kupata tiketi ya mechi za makundi.