TAHARIRI: Tuwachuje wanasiasa kwa makini mara hii
NA MHARIRI
KIPINDI cha pili cha mfumo wa ugatuzi kinapoelekea kukamilika kuna baadhi ya kaunti ambazo hazijaonja matunda ya utawala wa sampuli hii.
Mfumo wa ugatuzi umebainishwa na wataalamu kama bora zaidi katika kupeleka maendeleo katika maeneo ya mashinani.
Kukosekana kwa matunda ya ugatuzi kunatokana hasa na wanasiasa tunaowachagua kusimamia maeneo hayo.
Aghalabu wananchi hutumia vigezo hafifu kuwachagua viongozi wa siasa hasa magavana, wabunge na madiwani.
Lakini wasemavyo wahenga, heri kuchelewa kuliko kukosa.
Udhaifu huu unaweza kuondolewa hapo Agosti 9, ikiwa wananchi wenyewe watabadili mawazo yao kuhusu jinsi wanavyofanya maamuzi wakati wa uchaguzi.
Kampeni za siasa humu nchini zinapozidi kuvutia vitimbi na vichekesho vya kila aina kutoka kwa wanasiasa, wananchi nao wanafaa kumakinika kuhusu ujanja unaotumiwa ‘kuwafumba’ macho na hatimaye kuwachagua matapeli na watu laghai kuwawakilisha na kusimamia rasilimali zao.
Naam, inafahamika kuwa vitimbi na vichekesho hivyo kwa kawaida hutumiwa kuwavutia wananchi wahudhurie mikutano ya hadhara kwa wingi.
Hata hivyo, ubaya wake ni kuwa hii ni mbinu ambayo wakati mwingine huishia ‘kuwadanganya’ wapigakura ambao mwishoe huishia kuwachagua viongozi hao wachekeshaji badala ya wachapa kazi mamlakani.
Tungependa kutilia mkazo umuhimu wa wananchi kutathmini uwezo wa wanasiasa kuwaletea mabadiliko endapo watachaguliwa mamlakani, bila kuzingatia tu uwezo wao kuchangamsha umati katika kampeni.
Kwa msingi uo huo, vigezo vingine vya kitaaluma kama vile usomi au weledi wa kibiashara havitoshi kumfanya mtu aaminike kuwa na uwezo wa kuchapa kazi akichaguliwa kuwa kiongozi.
Tumeshuhudia mara nyingi watu waliodhaniwa watafanikisha maendeleo kwa msingi wa ufanisi wao katika nyanja nyinginezo wakiacha wananchi katika matatizo zaidi ya jinsi ilivyokuwa kabla wachaguliwe.
Litakuwa jambo la busara iwapo wananchi watakwepa mtego wa kufumbwa macho na wanasiasa wakati huu wa kampeni tunapoelekea kwa uchaguzi mkuu.
Kwa miaka mingi, wananchi wamekuwa wakijutia maamuzi yao punde tu baada ya kuchagua viongozi wa kisiasa.
Majuto hayo huwa hayasaidii, kwani sheria zilizopo kuhusu kuondoa kiongozi mamlakani, hasa kuondoa wabunge au rais, huwa ni vigumu mno kutekelezwa kabla miaka mitano ipite na uchaguzi mpya kuandaliwa.
Hivyo basi, ni heri raia wajitolee kikamilifu kuziba ufa badala ya kusubiri kujenga ukuta ifikapo wakati wa kuamua viongozi wanaotaka wawasimamie kwa miaka mitano ijayo.
Next article
Aubameyang afungia Barcelona mabao matatu katika mechi yake…