Connect with us

General News

UDA yatokwa na pumzi wawaniaji wakihamia Azimio – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

UDA yatokwa na pumzi wawaniaji wakihamia Azimio – Taifa Leo

UDA yatokwa na pumzi wawaniaji wakihamia Azimio

JAMES MURIMI, RUTH MBULA NA IAN BYRON

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto kinaendelea kupata pigo mashinani ikiwa imesalia miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Misukosuko kuhusu uteuzi imesababisha baadhi ya waliokuwa viongozi wa UDA kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhamia vuguvugu la Azimio la Umoja la Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga.

Katika Kaunti ya Laikipia, uhasama mkali wa kisiasa umeibuka baada ya Sammy Ndung’u msaidizi wa kibinafsi wa Mbunge wa Laikipia Mashariki, Amin Deddy kuchaguliwa kama mshirikishi wa UDA katika eneobunge hilo.

Mbunge wa zamani wa Laikipia Mashariki Mutahi Kimaru anadai hatua ya kumpa Bw Ndung’u wadhifa huo haikuwa haki.

Viongozi wa UDA wanaopinga hatua hiyo wanamtaka Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina aingilie kati ili aliyekuwa mshikilizi wa wadhifa huo Susan Kimiri aendelee kuwa usukani hadi muafaka upatikane.

Akizungumza katika hoteli moja mjini Nanyuki akiwa ameandamana na wanasiasa wa UDA, Bw Ndung’u alidai kuwa hiyo ni mbinu ya Bw Deddy kuvuruga uchaguzi wa chama hicho.

“Kama washikadau kwenye chama hiki hatukuhusishwa katika uteuzi wa Bw Ndung’u. Hiki ni chama chetu na lazima turuhusiwe kuwachagua viongozi wetu wala hatutaki udikteta katika chama hiki,” akasema Bw Kimaru.

Ushindani mkali unaendelea kushuhudiwa huku wanasiasa kadhaa wakijitosa ulingoni kuwania kiti cha eneobunge la Laikipia Mashariki. Waziri wa zamani wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Mbunge Mwakilishi wa Kike Cate Waruguru ni kati ya watakaogombea kiti hicho.

Katika kaunti jirani ya Nyandarua baadhi ya viongozi wamemshutumu Mbunge Mwakilishi wa Kike Faith Gitau kwa kujitwalia udhibiti wa chama hicho.

Mwanasiasa Moses Kiarie maarufu kwa jina ‘Badilisha’ ambaye pia analenga kiti cha Ugavana kupitia UDA kama tu Bi Gitau, amedai kuwa huenda mchujo wa chama hautakuwa huru iwapo Bi Gitau ataendela kuudhibiti.

Hata hivyo, Bi Gitau amemtaja Bw Kiarie kama mgeni chamani ikizingatiwa alijiunga nacho baada ya kuhama kile cha Chama cha Kazi (CCK) kinachoongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Mbunge huyo aliongeza kuwa anaonekana kuwa nyapara wa UDA Nyandarua kwa sababu ya kampeni kali aliyoendesha na kusaidia chama kushinda kiti cha udiwani wa Rurii mwaka jana.

UDA pia imepata pigo katika Kaunti ya Migori baada ya mwaniaji wake wa kiti cha Ugavana Jane Moronge na baadhi ya madiwani kuhamia mrengo wa Azimio la Umoja.

Bi Moronge alijiunga na chama cha DAP K kinachohusishwa na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na madiwani kadhaa wa kaunti hiyo wakajiunga na ODM. wakidai kuwa kuendelea kuwa UDA kunahatarisha nafasi zao za kuchaguliwa tena.