JUMA NAMLOLA: Ufahamu wa Kiingereza si mizani ya kupima werevu wa mtu
NA JUMA NAMLOLA
ULIMWENGU ulipokuwa umeanza kuvumbua viwanda, Wazungu walifika Afrika kuchukua watu wa kufanya kazi kwenye mashamba yao katika maeneo ya Carribean na Amerika Kusini.
Ndio sababu kuna Waafrika (watu weusi) katika nchi za Jamaica, Bahamas, Brazil, Cuba, Guyana, Haiti na hata Amerika Kaskazini. Wakati huo, Wazungu waliendeleza biashara ya utumwa kwa kisingizio kuwa Afrika lilikuwa ‘Bara Jeusi’.
Weusi wenyewe haukutokana na rangi ya watu bali kulikuwa na ujinga wa kupitiliza.Karibu karne mbili baadaye, ujinga huu unaendelea kwa Waafrika kujidharau kuwa hawaelewi lugha ya mtu aliyewanyanyasa.
Mwanamuziki wa Tanzania, Nasibu Abdul, maarufu Diamond, wiki hii amekejeliwa mitandaoni na Waafrika wenzake. Kisa na maana, eti hajui Kiingereza.
Diamond alikuwa ameulizwa kwa Kiingereza umri wake. Akajibu I am 31st badala ya I am 31.
Wajuaji mitandaoni walimcheka na kudai hakusoma, si mwerevu na hana ajualo.
Swali ambalo waliomkejeli wanapaswa kujibu ni hili: Tangu wajue hicho Kiingereza, kimewanufaisha vipi?
Diamond ametumia Kiswahili vyema na sasa hivi ni mmoja wa mabilionea wakuu Afrika Mashariki.
Muziki wake tangu siku akitumia Sharobaro Records hadi akaunda Wasafi Records, umemvunia umaarufu na pesa chungu nzima.
Werevu si kujua kusema Kiingereza. Werevu ni kutumia lugha ya mama au lugha asili kama Kiswahili, kuleta mabadiliko katika jamii.
Wavumbuzi wakubwa wengi ulimwenguni hawakuelewa Kiingereza. Guglielmo Marconi (Mtaliano) na Heinrich Hertz (Mjerumani) walibuni redio.
Rudolf Diesel (Mfaransa) alibuni injini inayotumia dizeli.
Mikhail Kalashnikov (Mrusi) alibuni bunduki ya AK-47.
Muhammad Al Khawarizmi (Muajemi) alianzisha hesabu za Algebra huku Fatma Al-Firhi (Mwarabu) akianzisha Chuo Kikuu cha kwanza duniani kilichotoa digrii.
Hawa wote hawakutumia Kiingereza kutekeleza ufanisi huo.
Kiingereza ni lugha tu na hata baadhi ya Waingereza hawakifahamu vyema. Kutokuza na kudharau lugha zetu, ndio ule ujinga uliofanya Wazungu watuite Dark Continent!