KULINGANA na Victor Okoth kutoka National Bee Institute, Kenya huagiza kutoka nje asilimia 70 ya asali inayotumika humu nchini.
Kauli ya mtaalamu huyu wa masuala ya nyuki, inaashiria kama taifa tuna uhaba mkubwa wa zao la asali.
Baringo, Ukambani, Mlima Elgon, Milima ya Aberdares, na Mlima Kenya yakiwa maeneo yanayoongoza katika ufugaji nyuki, asilimia 30 ya asali inayozalishwa nchini haitoshelezi mahitaji ya soko.
Kuziba mwanya uliopo, Okoth anasema Kenya hutegemea kwa kiasi kikubwa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan.
“Kama taifa tuna uwezo kuzalisha asali ya kutosha. Tuna raslimali itakayofanikisha ufugaji nyuki,” mdau huyo asema, akihimiza Wakenya kujiingiza katika shughuli za ufugaji wa nyuki.
Maeneo yanayozalisha matunda, Okoth anayataja kama kati ya yenye uwezo kufuga nyuki.
Kwa kawaida, mitunda huchana maua ishara ya kuanza kuunda matunda.
“Nyuki wanaridhia mazingira yenye maua, kufyonza juisi. Tukijumuisha mizinga katika mashamba na mabustani ya matunda, itasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na uhaba wa asali nchini,” Okoth aelezea.
Mukangu, kijiji kilichoko katika boda ya Kaunti ya Nyeri na Kirinyaga, Martin Mwangi na Samuel Muhindi wanatumia jukwaa la mashamba ya kahawa kufuga nyuki.
Kutoka kushoto, mfanyakazi wa Martin Mwangi na Samuel Muhindi ambao wanafuga nyuki katika kijiji cha Mukangu, Kiine, boda ya Nyeri–Kirinyaga. PICHA | SAMMY WAWERU
Eneo hilo pia ni tajika katika kilimo cha ndizi, maembe, karakara na maparachichi.
Yote, ni mimea inayochana maua.
Ni kutokana na jitihada za wawili hao, chini ya Walker Beekeepers wamezindua mradi na muungano wa kijamii, Mukandima, unaoshirikisha vijana, wajane na wasiojiweza kujiendeleza kimaisha.
Hatua hiyo ni mojawapo kubuni nafasi za ajira na kujipa pato la ziada.
Matumizi ya asali nchini yameongezeka hasa baada ya Kenya kukumbwa na janga la Covid-19 lililolemea vituo vya afya katika mataifa mengi ulimwenduni kote. Nchini Kenya kisa cha kwanza cha janga hili kiliripotiwa Machi 13, 2020.