Uhuru aelekezea Ruto makombora
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta ameanza kutumia mikakati aliyokuwa ameficha kumzuia naibu wake Dkt William Ruto katika juhudi zake za kushinda urais huku zikisalia siku 192 uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ufanyike.
Miongoni mwa mbinu hizo ni kupunguza umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya na katika ngome za kinara wa chama cha ODM Raila Odinga na kuanika kilichozua uhasama kati yake na naibu wake.
Rais Kenyatta anamuunga Bw Odinga anayegombea urais kwa mara ya tano kupitia vuguvugu la Azimio la Umoja linalotarajiwa kutangazwa kuwa muungano mkubwa wa kisiasa kabla ya Aprili 2022.
Kwa kuungana na zaidi ya vyama 15 vya kisiasa, vilivyomuunga Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, kiongozi wa nchi anatarajia umaarufu wa Dkt Ruto kushuka pakubwa uchaguzi mkuu ukikaribia.
Baadhi ya vyama hivyo ni Democratic Alliance Party Kenya (DAP-K), Maendeleo Chap Chap, Democratic Empowerment Party, Party of National Unity, Upya Party, Narc, The Young Democrats, Pan African Alliance (PAA) na Democratic Party miongoni mwa vingine.
Mnamo Alhamisi, Rais Kenyatta alitia saini sheria ya miungano ya vyama vya kisiasa inayolenga kufanikisha mikakati hii. Duru zinasema mazungumzo kati ya ODM na vyama vya Wiper na Kanu yameshika kasi katika juhudi za kumpiga jeki Bw Odinga kumshinda Dkt Ruto.
Rais Kenyatta alikuwa katika juhudi za kupatanisha Bw Odinga, Bw Musyoka, Bw Musalia Mudavadi, Bw Moses Wetangula na Bw Gideon Moi kabla ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kusambaratika.
Mazungumzo hayo yamefufuliwa baada ya Bw Mudavadi na Wetangula kuungana na Dkt Ruto.
Washirika wa Rais Kenyatta wanasema kwamba anapanga kampeni kali hadharani na hata ‘chini ya maji’ ili kuimarisha umaarufu wa Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya na maeneo ambayo Dkt Ruto na washirika wake katika muungano wa Kenya Kwanza amevamia.
Kuanzia Februari, Rais Kenyatta anatarajiwa kukutana na viongozi wa eneo la Mlima Kenya kuachilia kombora kali kuhusu chanzo cha uhasama wake wa kisiasa na Dkt Ruto. Mikutano hiyo itakuwa katika ikulu ndogo ya Sagana.
“Litakuwa kombora ambalo litabadilisha siasa za eneo la Mlima Kenya. Rais Kenyatta ameamua kwamba wakati umefika wa kufungua moyo wake kwa Wakenya. Kumbuka amewahi kudokeza kuwa hataachia nchi watu wanaogawanya Wakenya,” alisema mbunge mmoja wa Kaunti ya Kiambu aliyeomba tusitaje jina asionekane kumwaga mtama.
Mbunge huyo anasema kwamba kiongozi huyo wa nchi amejipanga kuhakikisha ameacha Kenya katika mikono salama.
Baada ya Dkt Ruto kuungana na Bw Mudavadi na Wetangula wiki moja lililopita, Rais Kenyatta alikunjua kucha zake na kuhakikisha kuwa washirika wa makamu huyo wa rais wa zamani wamemtema na kujiunga na chama cha DAP- Kenya kinachounga kampeni ya Azimio la Bw Odinga.
Wabunge watano na Gavana wa Bungoma, Wycliffe Wangamati walihama ANC baada ya kukutana na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi. Kuhama kwa wabunge hao Peter Nabulindo (Matungu), Tindi Mwale (Butere), Titus Khamala (Lurambi), Oku Kaunya (Teso North) na Ayub Savula (Lugari) kulimtoa pumzi Bw Mudavadi na chama chake.
Wanamikakati wa Rais Kenyatta wanasemekana kuwa katika hatua za mwisho za kuhakikisha hali kama hiyo inatokea maeneo mengine nchini ili kubadilisha kabisa mawimbi ya siasa.