Uhuru akuza wanasiasa kizazi kipya Mlimani
NA ONYANGO K’ONYANGO
RAIS Uhuru Kenyatta anapanga kukuza kizazi kipya cha viongozi katika ngome yake ya Mlima Kenya huku akikaribia kuondoka afisini baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Inasemekana kuwa Rais Kenyatta anapania kuwasaidia wanasiasa kutoka eneo hilo ambao hawajakuwa katika siasa kwa zaidi ya mwongo mmoja ili waweze kuendeleza ajenda zake atakapostaafu.
Kwa kufanya hivyo, Rais Kenyatta anafuata mfano wa aliyekuwa Waziri marehemu John Michuki, aliyechangia pakubwa katika kumwelekeza nyakati za utawala wa rais mstaafu Mwai Kibaki.
Aidha, kiongozi wa taifa anaonekana kufuata mfano wa Naibu wake William Ruto ambaye amekuwa akiwalea wanasiasa chipukizi ili waendeleze ajenda zake na kuendesha uasi dhidi ya serikali.
Tangu 2018, Dkt Ruto alipiga kambi katika eneo la Mlima Kenya hali iliyomsaidia kuwaelekeza kisiasa wanasiasa kama vile wabunge Ndindi Nyoro (Mbunge wa Kiharu), Alice Wahome (Kandara), Rigathi Gachagua (Mathira), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), miongoni mwa wengine.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta anataka kuwakuza kisiasa wabunge kama vile Kanini Kega (Kieni), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Sabina Chege (Mwakilishi wa Kike, Murang’a), Jeremiah Kioni (Ndaragua ) na mmoja wa manaibu kiongozi wa Jubilee Kinoti Gatobu.
Kiongozi wa taifa anataka kuwatumia wanasiasa hao kudhibiti wimbi la chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambalo limekita katika ngome yake ya Mlima Kenya.
Bw Kioni amekwezwa kwa kutunukiwa wadhifa wa Katibu Mkuu wa Jubilee ilhali Bw Kega amepandishwa ngazi na kupewa cheo cha Mkurugenzi wa Uchaguzi katika chama hicho tawala.
Jana, Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Joshua Kutuny aliambia Taifa Leo kwamba kando na kuendesha ajenda zake za kisiasa, wanasiasa hawa watamsaidia Rais kuvumisha azma ya urais ya kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Mlima Kenya.
Mabadiliko hayo yanajiri wakati ambapo Jubilee ilikuwa inakabiliwa na tishio la kuangamia haswa katika eneo lote la kati mwa Kenya, kutokana na kupanda kwa umaarufu wa UDA.
Bw Kega alitetea hatua hiyo ya Rais Kenyatta kuteua kizazi kipya cha viongozi wa kisiasa akisema wanasiasa hao wako na nguvu na uwezo wa kuendeleza ajenda zake.
“Mimi sioni kwamba Rais anatulea kisiasa. Tumekuwa wakakamavu na wenye bidii katika kuuza sera na maongozi ya Jubilee kuanzia mashinani hadi ngazi za kitaifa. Tumejitolea kuendeleza ajenda zake kwa manufaa ya watu wetu. Tumekuwa waaminifu zaidi tangu chama cha Jubilee kilipoundwa mnamo Septemba 16,2016,” akasema Bw Kega ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti.
Alisema wajibu wake mkubwa wakati huu ni kuhakikisha kuwa Jubilee inashinda viti vingi katika Bunge la Kitaifa, Seneti, Baraza la Magavana na mabunge ya kaunti.
“Pia kazi yetu kubwa ni kumnadi kiongozi wa ODM Raila Odinga ili aweze kushinda urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” Bw Kega.
Next article
ZARAA: Uzito na utamu wa matikitimaji anayokuza umempatia…