Uhuru aliwapuuza waliotaka nishtakiwe kwa kosa la uhaini – Raila
Na CHARLES WASONGA
HATIMAYE kiongozi wa ODM amefichua kuwa ni Rais Uhuru Kenyatta aliyemwokoa kutokana na hatari ya kushtakiwa kwa kosa la uhaini baada ya kujiapisha kuwa “Rais wa Wananchi”.
Bw Odinga alikula kiapo hicho mchana hadharani katika bustani ya Uhuru Park mnamo Januari 30, 2018 kuonyesha kuwa hakutambua kuashiria kupinga uhalali wa ushindi wa Rais Kenyatta katika marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017.
Alilishwa kiapo hicho na mwanaharakati Miguna Miguna, Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang wakisaidiana na Seneta wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Makadara George Aladwa.
Akiongea na waumini katika Kanisa la Legio Maria katika mtaa wa Makongeni, Nairobi, Jumapili Novemba 7, Bw Odinga alifichua kuwa wandani wa Rais Kenyatta walitaka ashtakiwe kwa uhaini kwa kujiapisha kinyume cha sheria.
Bw Odinga alisema kiongozi wa taifa alipuuzilia mbali shinikizo hizo na badala yake akaamua kufuata mkondo wa maridhiano.
“Hii ndio ilichangia salamu za heri kati yangu na Rais Kenyatta nje ya jumba la Harambee, kitendo maarufu kama handisheki,” akasema.
Akaongeza: “Uhuru aliambiwa kwamba nimevuka mpaka na kwamba kula kiapo ilikuwa sawa na uhaini. Walimwambia kwamba nilifaa kushtakiwa na kunyongwa katika gereza la Kamiti.”
Bw Odinga alisema yeye na Rais Kenyatta walifanya handisheki baada ya kutambua kuwa taifa lilikuwa likipitia hali ngumu na lilihitaji maridhiano ya kisiasa.
“Tulitambua kuwa umoja wa taifa hili ni muhimu zaidi kuliko masilahi yetu ya kisiasa kama viongozi wa mirengo ya Jubilee na Nasa,” akaeleza.
Baada ya Bw Odinga kula kiapo katika Uhuru Park, washirika wake kama vile T J Kajwang na Aladwa walikamatwa na kustakiwa kwa kosa la kuongoza mkutano haramu.
Naye Bw Miguna Miguna alizuiliwa katika kituo cha Polisi cha Kajiado kisha akasafirishwa kwa nguvu hadi Canada.
Maafisa wa usalama walidai kuwa hakuwa na kibali cha kuwa nchini kwa sababu “ni raia wa Canada”.
Vile vile, ilidaiwa mwanaharakati huyo ambaye ni wakili, hakuwa amepata uraia mpya wa Kenya baada ya ‘kuuasi’ miaka kadha iliyopita.
Next article
Wachungaji wapendekeza adhabu ya kiboko irejeshwe shuleni