Uhuru asitisha shughuli zote za usoroveya mtaani Mukuru
Na MARY WAMBUI
RAIS Uhuru Kenyatta amesimamisha shughuli zote za ardhi katika maeneo ya vitongoji duni vya Mukuru kwa Njenga ambapo mwanaume mmoja alipigwa risasi Sikukuu ya Krismasi usiku baada ya watu wasiojulikana kuanza kufanya usoroveya wa ardhi.
Aidha, ameamrisha kufidiwa mara moja kwa wahasiriwa wote waliofurushwa kutoka vitongoji duni hivyo usiku huo ambapo watu wengine wawili walipata majeraha ya risasi.
Mtu mmoja alipigwa risasi tumboni kufuatia makabiliano makali baina ya polisi na watu waliofurushwa. Shughuli zilizositishwa zinajumuisha usoroveya wa karibu ekari 100 za ardhi na kufurushwa kwa takriban watu 40,000 waliokuwa wakiishi katika kambi za hema kwenye ardhi hiyo inayozozaniwa inayodaiwa kumilikiwa na shirika la kibinafsi.
“Usoroveya na mambo yote mengine yatashughulikiwa na serikali ili kuepuka unyanyasaji kutoka kwa mashirika ya mabwenyenye,” Waziri Fred Matiang’i aliamrisha jana baada ya kukutana na wazee wa Nyumba Kumi katika jamii hiyo.
Katika muda wa mwezi mmoja, wizara husika zitahitajika kuharakisha majadiliano na wamiliki hao wa ardhi wanaozingirwa na utata, viongozi wa kijamii na pande zote husika, kufanya usoroveya wa ardhi ili kubaini ukubwa wake halisi na kuhesabu idadi ya waliofurushwa makwao kabla ya kuwapa makao jinsi ilivyopangwa.
“Tunataka kila mtu ambaye kwa sasa amefurushwa makwao kurejea mara moja. Maagizo ni kwamba tusitishe mara moja kila shughuli Mukuru Kwa Njenga hadi kila mtu atakapopatiwa makao,” alisema Bw Matiang’i.
Mkutano huo uliofanyika katika Kanisa la Mariakani Church of God, ulihudhuriwa vilevile na waziri mwenzake wa Ardhi, Farida Karoney, Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho, Katibu wa Usalama wa Ndani Wilson Njega, Mkuu wa Halmashauri ya Utoaji Huduma Nairobi Luteni Jenerali Mohammed Badi, Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai miongoni mwa maafisa wengine.
Matokeo ya ufurushaji na ghasia za kikatili mnamo Jumapili usiku yalimvutia Rais Kenyatta aliyeripotiwa kuzuru eneo hilo na kuzungumza na wakazi mnamo Disemba 27.
Kamanda wa Polisi katika Jiji la Nairobi Augustine Nthumbi na Kamanda wa Polisi Embakasi Bw John Nyambu wameamrishwa kwenda likizo ya lazima ili kutoa nafasi kwa Kitengo cha Masuala ya Ndani kuchunguza mchango wao kwenye ubomoaji huo.
Wawili hao wamekwishahojiwa na kuandikisha taarifa zao.Mwingine aliyehojiwa pia ni Afisa wa pili kuhusu usimamizi wa shughuli katika NMS, Dkt Mark Leleruk.
Next article
Kaunti 22 zilivyotafuna hela za wananchi