Uhuru kuachia kila raia deni la Sh260,000
Na CECIL ODONGO
RAIS Uhuru Kenyatta ataachia kila Mkenya deni la Sh260,000 atakapostaafu siasa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Hii ni baada ya kubainika kuwa serikali inalenga kupandisha kiwango cha juu zaidi cha deni la taifa kutoka Sh9 trilioni hadi Sh13 trilioni.
Bunge la kitaifa wiki hii lilitaka kiwango hicho kipandishwe ili serikali iwe na nafasi ya kukopa Sh846 bilioni kujaza kiasi kinachopungua kwenye bajeti ya 2022/23.
Jumla ya deni la Kenya kwa sasa ni Sh7.99 trilioni na litakuwa Sh8.6 trilioni kufikia Juni 2022.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Amos Kimunya wiki hii aliwasilisha marekebisho kwenye sera ya kuandaa bajeti na sasa Hazina Kuu ya Kifedha itakumbatia mabadiliko hayo ili kupandisha kiwango cha deni la kitaifa.
Akiwasilisha marekebisho hayo bungeni, Bw Kimunya hata hivyo, alikosa kufichua kiwango cha juu zaidi ambacho Kenya itaruhusiwa kukopa ila duru kutoka Bunge zinaarifu kuwa kiasi hicho kitapandishwa hadi Sh13 trilioni.
Bajeti ya mwaka wa 2022/23 ni Sh3.33 trilioni ambayo itakuwa kiwango cha juu zaidi tangu Kenya ijinyakulie uhuru.Mnamo 2019 wabunge walipandisha pesa ambazo Kenya inaweza kukopa kutoka Sh6 trilioni hadi Sh9 trilioni na kihesabu iwapo itaongezwa hadi Sh13 trilioni, basi kila Mkenya atakuwa akidaiwa Sh260,000.
Kutokana na hilo, Hazina Kuu ya Kifedha sasa itapendekeza marekebisho kwenye sheria ya usimamizi wa fedha za umma kisha iwasilishwe bungeni ndipo ifanyiwe mabadiliko.
“Kamati ya bajeti inaiomba Hazina Kuu ya Kifedha kupandisha kiwango cha deni la taifa ili kuiwezesha kutekeleza mahitaji yote kwenye bajeti yake na pia kufaulisha mbinu za kukusanya fedha,” akasema Bw Kimunya.
Wabunge walipitisha mapendekezo ya Bw Kimunya, hii ikiwa na maana kuwa afisi ya Rais itatengewa Sh2 trilioni, Sh38.4 bilioni zikielekezwa kwa Bunge la Kitaifa/ Seneti, Sh18.8 bilioni kwa idara ya mahakama huku kaunti zikitengewa mgao wa Sh370 bilioni.
Wakati wa kikao kilichoandaliwa bungeni, wabunge wanaoegemea upande wa Naibu Rais, Dkt William Ruto walipinga vikali kupandishwa kwa kiwango cha pesa ambazo nchi inaweza kukopa.
Serikali imekuwa ikidai kuwa Kenya ina uwezo wa kuyalipa madeni yake baada ya raia kuonekana kukerwa na mtindo wa kukopa mara kwa mara ilhali sehemu kubwa ya fedha hizo zimekuwa zikiishia mikononi mwa viongozi wafisadi.
Kwa upande mwingine serikali inasisitiza kuwa pesa ambazo zinakopwa zinalenga kutumika kumaliza miradi iliyoanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta ambayo lazima ikamilishwe kabla hajaondoka afisini.
Wiki hii Naibu Rais na vinara wenzake Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula walilalama kuwa kiwango cha deni la taifa kiko juu zaidi, matamshi ambayo yalilenga kuzuia Bw Kimunya kulirai bunge kubadilisha mapendekezo ya ripoti ya kamati ya fedha bungeni.
Next article
Wakazi walilia kaunti imalize uvamizi wa ndovu na viboko