UhuRuto sasa watishia kuanza kupakana tope
NA LEONARD ONYANGO
RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wametishia kupakana tope hadharani huku siasa za kuchafuliana majina zikionekana kushika kasi nchini.
Kulingana na viongozi wa Jubilee, Rais Kenyatta anajiandaa kuzuru eneo la Mlima Kenya ambapo wandani wake wanasema atafichua “maovu ya naibu wake” na kuwaelezea wakazi kiini cha kutengana kwao.
Kulingana na Mbunge wa Nyeri Mjini, Wambugu Ngunjiri, Rais Kenyatta anatarajiwa kufichua siri ‘nzito’ ya Dkt Ruto kuhususu “maovu aliyotenda” tangu walipochukua hatamu za uongozi 2013.
Mabwanyenye wa Mlima Kenya walipoidhinisha rasmi kuunga mkono kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga mnamo Disemba mwaka jana, pia walitishia kufichua men – gi kuhusu Ruto.
Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, Rais Kenyatta alirusha tope la kwanza kwa naibu wake alipodai Dkt Ruto alikuwa waziri wa kilimo wakati viwanda vya sukari katika eneo la magharibi mwa Kenya vilipoporomoka.
“Leo ninazomewa kuhusu kuporomoka kwa viwanda vya sukari vya Mumias na Nzoia. Wakati viwanda hivyo viliporomoka, mimi sikuwa rais. Yeye (Ruto) ndiye alikuwa waziri wa kilimo,” Rais Kenyatta akaambia kundi la vijana waliokongamana katika Ikulu ya Nairobi.
Rais Kenyatta pia alionekana kuhusisha naibu wake na masaibu ya Shirika la Nyama nchini (KMC) ambalo alisema kuwa lilikuwa likichinja ng’ombe 30 kwa mwezi Dkt Ruto alipokuwa waziri wa kilimo.
“Lakini sasa KMC inachinja ng’ombe 300 kwa siku,” akasema Rais Kenyatta.
Dkt Ruto alikuwa waziri wa kilimo katika serikali ya Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki. Rais Kenyatta alisema kuwa alikuwa na kibarua kigumu kuendesha serikali kati ya 2013 na 2017 ambapo Dkt Ruto alikuwa na ushawishi mkubwa serikalini.
Katika mkutano wa kisiasa uliofanyika katika Kaunti ya Baringo, Jumapili, wandani wa Dkt Ruto nao walitishia kufichua siri za Rais Kenyatta iwapo atathubutu kufichua za kion – gozi wao.
Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale alidai kuwa serikali ya Rais Kenyatta “imefanya maovu mengi” ambayo wataweka wazi iwapo atamwanika Dkt Ruto.
“Acha kujificha na kusema ati utaambia watu yale Ruto amefanya. Thubutu kufichua siri za Ruto, na – si tutafichua maovu ya serikali yako.
Sisi ambao tulifanya kazi na wewe tunakujua ndani na nje. Rais usitutishe!” Akasema Bw Duale.
Mbunge huyo pia alidai kuwa Rais Kenyatta amegawanya nchi kwa kufadhili kubuniwa kwa vyama vidogo vya ‘kikabila’.
“Rais wewe ndiye unafadhili kuundwa kwa vyama vya kikabila kwa
lengo la kugawanya Wakenya. Halafu unatudanganya kwamba unataka kuacha nchi ikiwa imeungana,” akadai Bw Duale.
Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata anasema kuwa hatua ya Rais Kenyatta kutisha kumchafulia jina naibu wake haitasaidia kubadilisha msimamo wa kisiasa wa wafuasi wake.
Lakini wadadisi wanasema kuwa Rais Kenyatta huenda akafaulu kubadili mawazo ya baadhi ya wakazi wa Mlima Kenya iwapo atafichua si – ri za Dkt Ruto.
“Kambi ya Ruto huenda inajua mambo ambayo Rais Kenyatta anataka kufichua na hiyo ndiyo maana wanamrushia cheche za maneno ili wakazi wa Mlima Kenya wasimwamini,” anasema Mtaalamu wa Mawasiliano Javas Bigambo.
Bw Bigambo pia anasema kuwa cheche hizo za wandani wa Dkt Ruto zinalenga kumaliza nguvu ziara ya Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya.
Next article
ICC: Yadaiwa Gicheru alitoa hongo ya mamilioni kwa mashahidi