Connect with us

General News

Uhusiano wa Ruto, Yebei waibuka ICC – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Uhusiano wa Ruto, Yebei waibuka ICC – Taifa Leo

Uhusiano wa Ruto, Yebei waibuka ICC

NA VALENTINE OBARA

KESI inayomwandama wakili Paul Gicheru katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), huenda ikafichua mengi kuhusu kifo cha Meshack Yebei takriban miaka saba iliyopita.

Hii ni baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa wakili huyo alikiri kukutana na Yebei, na kwamba walikuwa washirika katika njama za kumwokoa Naibu Rais William Ruto kutoka kwenye kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Stakabadhi mpya ambazo upande wa mashtaka umewasilisha mahakamani zinadai kuwa Bw Gicheru alihojiwa na maafisa wa ICC mnamo 2018, miaka miwili kabla ya kujisalimisha.

Hati hiyo iliyotiwa sahihi na Naibu Kiongozi wa Mashtaka, James Stewart, inaonyesha pia Bw Gicheru alikiri kuwahi kuwasiliana na kukutana na baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi dhidi ya Dkt Ruto.

Vile vile, Bw Stewart amedai kuwa wakili huyo aliyekuwa na afisi Eldoret, alisoma pamoja na Dkt Ruto katika Shule ya Upili ya Kapsabet, kuashiria kuwa walifahamiana vyema.

Yebei aligonga vichwa vya habari alipotoweka baada ya kutekwa nyara Desemba 28, 2014 eneo la Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu. Mwili wake ulipatikana Januari 2015 katika mbuga ya wanyama ya Tsavo, Taita Taveta.

Upande wa mashtaka unadai una ushahidi kuthibitisha kuwa Dkt Ruto alitumia mamilioni ya pesa kufadhili mipango ya kuhonga mashahidi ili wajiondoe na hivyo kuvuruga kesi hiyo.

Ingawa haijafahamika wazi kilichompelekea Bw Gicheru kukubali kuhojiwa na ICC mnamo 2018, upande wa mashtaka umeiomba mahakama ikubali rekodi za mahojiano hayo zitumiwe kama ushahidi dhidi yake.

“Ijapokuwa mshtakiwa alikana madai mengi aliyoulizwa wakati wa mahojiano, rekodi hizi zinahusiana sana na kesi kwa vile ni maelezo yake mwenyewe.

“Haya yatatoa kigezo muhimu ambacho ushahidi mwingine wowote au taarifa inaweza kulinganishwa nayo na pia inapunguza hatari ya mshtakiwa kubadili ushahidi wake na hivyo basi mahakama itasaidika kubainisha ukweli,” ikasema hati hiyo ya upande wa mashtaka.

Zaidi ya hayo, imesemekana wakili huyo alikiri kuwa alisaidia mashahidi kunakili hati za kisheria za kujiondoa katika kesi ya Dkt Ruto wakati alipohojiwa.

Bw Gicheru alijisalimisha katika ICC mnamo Novemba 2, 2020 baada ya agizo la kukamatwa kwake kutolewa Septemba 10, 2015.

Kufikia sasa, baadhi ya mashahidi ambao upande wa mashtaka ulitaka kutegemea katika kesi dhidi ya Bw Gicheru wamesitasita kujiwasilisha mahakamani, huku wengine wakisemekana hawajulikani waliko.

Endapo mahakama itakubali ombi la upande wa mashtaka kujumuisha rekodi za mahojiano aliyofanyiwa Bw Gicheru mnamo 2018 kama ushahidi, madai dhidi yake huenda yakapigwa jeki.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba kuruhusiwa kutumia rekodi za mahojiano ambayo mashahidi walifanyiwa kabla watoweke, lakini ombi hilo likapingwa na mshtakiwa kupitia kwa wakili wake, Bw Michael Karnavas

“Gicheru alifahamishwa kwamba alikuwa na haki ya kukataa kusema chochote kinachoweza kumfanya apatikane na hatia kabla ahojiwe, lakini bado akaamua kuhojiwa bila kuwa na wakili wake kwa hivyo sasa hawezi kuja kusema hajatendewa haki,” Bw Stewart akaeleza.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending