MAKALA MAALUM: Ulevi ulivyompokonya kazi ya polisi pamoja na familia
WANGU KANURI na LEONARD ONYANGO
KILA mara shule zilipofungwa mwishoni mwa muhula, John Mwangi Wakahora, alijawa na bashasha kwani alijua hiyo ilikuwa fursa mwafaka ya kubugia mvinyo aina ya muratina na busaa.
Bw Wakahora, 54, anasema kuwa alianza kubugia mvinyo akiwa na umri wa miaka 10 nyumbani kwao katika eneo la Nyahururu, Kaunti ya Nyandarua.
Matokeo ya mtihani wa kukamilisha elimu ya msingi yalipotoka, Wakahora alikuwa miongoni mwa watahiniwa waliofanya vibaya zaidi.
“Mbali na kutotia bidii masomoni, nilikuwa nikilewa chakari. Hivyo kufeli mtihani hakukunishtua,” anasema Bw Wakahora.
Alikuwa mlevi chakari kiasi kwamba alitumia fedha alizopewa kutoa sadaka kanisani Jumapili kununua pombe.
Anasema kuwa alijifunza ubugiaji wa pombe kutoka kwa kijakazi wa mjomba yake.
Licha ya kupata alama za chini, John alijiunga na shule ya upili lakini marafiki aliotangamana nao walikuwa waraibu kama yeye.
“Mimi na marafiki zangu tulikuwa tunatoroka shuleni kunywa chang’aa na kuvuta bangi. Cha kushangaza sikuwahi shikwa.”
Ili kutosheleza kiu yake ya dawa za kulevya shule zilipofungwa, John alikuwa akiiba mahindi, maharagwe na maziwa yaliyowekwa ghalani na kupata mapeni kidogo.
Weledi wake katika soka, hata hivyo, ulimfanya kupewa cheo cha kiranja shuleni. Lakini alitumia kipaji hicho kusaka hela za kununua pombe badala ya kujisaidia katika maisha ya usoni.
“Shule zilipokuwa zikifunguliwa, mimi na marafiki zangu tulikuwa tukipatana Nyahururu na kubugia pombe na kuvuta bangi. Siku hizo hakukuwa na masharti ya kufika shuleni kwa saa fulani ili muradi tu ufike shuleni,” anaeleza.
Siku moja, baada ya kuibuka mshindi wa soka wilayani Nyahururu, John alisherehekea kwa kunywa chang’aa.
Mwalimu mkuu aliponusa pombe, John alimweleza hakuwa amelewa na akaachana naye.
“Heri mwalimu huyo angenifukuza bila ya kuangalia umaarufu nilioletea shule ile. Kufukuzwa kule kungekuwa funzo kwangu kuwa pombe si nzuri,” anajutia.
Nyumbani, babake John alianza kumshuku mwanawe huku akimwonya bila mafanikio.
Alipofanya mtihani wake wa kidato cha nne, John hakupita lakini wazazi wake walimtafutia shule ya kujiunga nayo ili asome kidato cha tano na sita.
Shuleni humo, John alifanywa kiongozi wa michezo na akawa akishirikiana na mwenzake wa maabara kunywa kemikali ya ‘ethanol’ kukata kiu cha pombe.
“Kila wikendi tulikuwa tunakunywa ethanol kwa kuichanganya na maji.”
Baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha sita, John hakupita mtihani na aliajiriwa na wazazi wake kufanya kazi katika duka lao.
Pale dukani, John alikuwa akiwaibia wazazi wake na baada ya miezi miwili duka hilo liliporomoka. Pesa alizoiba ziliishia kwenye ununuzi wa pombe ili kukata kiu yake ambayo haikuwa ikiisha.
Mnamo 1990, aliajiriwa kuwa afisa wa polisi na kuanza kufanya kazi katika eneo la Gigiri, Nairobi.
Miezi michache baada ya kuoa mnamo 1995, ndoa yake ilianza kukumbwa na msukosuko kutokana na ulevi.
“Nilitumia fedha zangu katika ulevi na kumwachia mke wangu majukumu yote ya nyumbani,” anaeleza.
Ndoa yake hatimaye ilivunjika miaka tisa baadaye.
Kazini, John alihamishwa hadi kituo cha polisi cha Wajir na baada ya mwezi, aliomba ruhusa na kurudi nyumbani kwa miezi mitatu.
Hata hivyo, John alikosa kurejea kazini kwa miaka mitatu lakini aliendelea kulipwa mshahara na kutumia hela hizo kunywa pombe.
Mnamo 2007, John alikamatwa na polisi akishukiwa kujihusisha katika uhalifu.
Uchunguzi ulibaini kuwa John alikuwa mwenzao lakini aliacha kazi bila kufuata utaratibu uliopo. Alitimuliwa kutoka kikosini na vitu vyake kutolewa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Wajir.
Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, hatimaye alipata usaidizi na kupelekwa katika kituo cha kubadili tabia ambapo alitibiwa na kuacha pombe miaka 12 iliyopita.
Takwimu za Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (Nacada) zinaonyesha kuwa asilimia 14 ya Wakenya wa umri wa kati ya umri wa miaka 15 na 64 wanakunywa pombe humu nchini.
Kulingana na Nacada, asilimia nane ya watoto wa kati ya umri wa miaka 10 na 14 wamewahi kuonjeshwa pombe zaidi ya mara moja. Wengi wao wameonja pombe aina ya chang’aa.
Tafiti zimeonyesha kuwa watoto wanaonjeshwa pombe baadaye hugeuka kuwa walevi chakari wanapokuwa watu wazima.
Utafiti uliofanywa nchini Australia na ripoti kuchapishwa katika jarida la Lancet Public Health, ulibaini kuwa watoto wanaoonjeshwa pombe huwa vigumu kuacha.
“Hali ni mbaya zaidi watoto hao wanapoonjeshwa pombe na wazazi wao. Kwanza, wanachukulia kuwa wazazi wamewaruhusu kubugia pombe. Pili, wanajenga uraibu hivyo huwa vigumu kwao kuacha,” ikasema ripoti hiyo ya utafiti.