DOUGLAS MUTUA: UN sasa ifanye mabadiliko ili kutambua bara la Afrika
Na DOUGLAS MUTUA
BARA la Afrika, ambalo limekaliwa mguu wa kausha na Wazungu tangu enzi ya biashara ya watumwa, limeanzisha mwamko mpya wa kukataa kudhulumiwa huku likiwa kimya.
Muungano wa Afrika (AU) umeunda jopo la mataifa 10 ambayo yanashinikiza Umoja wa Mataifa (UN) ufanye mabadiliko ili kulitambua na kuliheshimu bara hili.
Mataifa hayo ni Kenya, Uganda, Senegal, Zambia, Sierra Leone, Congo-Brazzaville, Libya na Namibia.
Miongoni mwa mabadiliko ambayo yanasisitiza ni sharti yafanyike ni lile la kulipa angaa taifa moja la Afrika uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama.
Kikawaida, baraza hilo huwa na mataifa wanachama 15, ila ni matano pekee ambayo yana uanachama wa kudumu, sikwambii nguvu kupita kiasi katika maamuzi yote ya UN.
Yaliyo na hadhi ya kudumu, na ambayo yana kura ya turufu yenye nguvu hivi kwamba moja tu likipinga kitu hakifanyiki, ni Marekani, Urusi, Uchina, Ufaransa na Uingereza.
Waasisi wa mabadiliko wanasema kuwa orodha hiyo fupi ni dhalimu kwa Afrika kwa kuwa maamuzi mengi ya baraza hilo la usalama huiathiri Afrika zaidi ilhali haina mwakilishi.
Maamuzi mengi ya baraza lenyewe huhusu amani na usalama, hivyo kila wakati maamuzi hufanywa kuhusu Afrika bila bara lenyewe kushirikishwa kwa vyovyote vile.
Siasa za kimataifa zilivyo ni kwamba mataifa yaliyo na kura ya turufu yamefanya urafiki wa mengine yasiyo na kura hiyo, hivyo maslahi ya yasiyonayo hutetewa kikamilifu.
Hivyo ndivyo ambavyo, kwa mfano, taifa la Israel limeweza kufanya mambo mengi ya kimaendeleo na kiusalama bila kuzuiwa na UN.
Hakuna taifa la Afrika ambalo lina rafiki kama huyo; mara nyingi likiwasilishwa lolote la kutuadhibu huungwa mkono kwa asilimia zote, Mwafrika akasubiri kiboko kama mtoto mkorofi.
Baraza hilo lingekuwa na mwanachama mmoja pekee kutoka Afrika angekuwa akipiga kura ya turufu dhidi ya maamuzi yanayolidhulumu bara letu. Mmoja pekee anatosha!
Hiyo ni hujuma ambayo inaendelezwa na mataifa waanzilishi wa UN yakiungwa mkono na mengine ambayo tayari yana watetezi kwenye baraza hilo lenye nguvu.
Mataifa hayo matano hayaoni aibu ya bara zima la Afrika lenye watu takriban 1.4 bilioni kukosa mwakilishi.
Baraza la Usalama la UN litatia akili pale Muungano wa Afrika (UN) utakapopitisha azimio la kuondoka kwenye Umoja wa Mataifa na kuipa nguvu zaidi AU kutetea Afrika kimataifa.
Afrika ikianza kutetea maslahi yake kwa pamoja, watesi wake watanywea na kukubali mabadiliko hayo ambayo yanahitajika kwa dharura.
[email protected]
Next article
TAHARIRI: Bila kukuza soka yetu tusahau nafasi za bara Ulaya