KATIKA miji mingi mikubwa nchini, wafanyabiashara wa uchukuzi wa umma hurembesha sana vyombo vyao vya uchukuzi.
Vyombo hivyo vinavyojumuisha matatu, mabasi, tuktuk na pikipiki hupambwa kwa njia mbalimbali hasa kwa michoro na maandishi.Haya hufanywa kwa vile huwa inaaminika mapambo huvutia wateja kushinda kile ambacho hakijarembeshwa.
Imani hii imewasukuma wamiliki wa punda katika Kaunti ya Lamu pia kuamua kurembesha wanyama hao ambao hutegemewa sana kwa uchukuzi katika maeneo mbalimbali ya mji huo wa kale tangu jadi.
Kando na kugeukia ubunifu huo wa kuwarembesha punda wao kuwavutia watalii, wageni na hata wenyeji, imebainika ubunifu huo pia umeanza kuvutia wanasiasa ambao wanapamba punda kwa nembo zao katika msimu huu wa kampeni.
Unapotembea kwenye vishoroba vya mji wa Lamu, si ajabu kumpata punda akiwa amevalishwa mavazi ya rangi ya kuvutia, herini, shanga, kofia au hata kupakwa rangi mdomoni, kwenye kope na hata kwato, ilmradi uvutiwe kumkodi mnyama huyo.
Wahudumu waliohojiwa na Taifa Leowalibainisha kuwa, watalii huwa wanakodi punda wa kawaida ili kujivinjari kisiwani Lamu.
Wao hulipishwa ada tofauti kulingana na muda ambao wanataka kumtumia punda huyo.Bw Mohamed Omar ambaye ni mmiliki wa punda kisiwani Lamu, alisema wakati wa msimu mkuu wa utalii, yeye hupata hadi Sh2,000 kwa siku kupitia juhudi zake za kumrembesha punda na kumkodi kwa watalii kisiwani.
“Hapa ilibidi kuibuka na ubunifu huu wa kurembesha punda wetu ili kupata biashara. Watalii wamekuwa wachache kutokana na hali ya kiusalama eneo hili na pia janga la corona. Badala ya kutegemea biashara ya kubeba mizigo ambayo pia imepungua, ilibidi kutafuta jinsi tutawavutia hawa watalii kukodi punda wetu. Nashukuru kwamba kwa sasa biashara inanoga. Angalau tunapata mtaji wa kukimu familia zetu,” akasema Bw Omar.
Mmiliki mwingine, Bw Fadhil Abbas, aliye katika mtaa wa Mkomani mjini Lamu, anasema mbali na kuwavutia watalii, ni kupitia kuwapamba punda ambapo pia amekuwa akijizolea zawadi kutoka kwa wahisani na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za wanyama.
Mnamo Mei 8, 2018 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Punda Ulimwenguni, Bw Abbas alituzwa kwa kuibuka mmiliki wa punda mwenye tajiriba bora zaidi ya kumrembesha na kumtunza punda.
“Urafiki niliojenga na punda wangu umeniwezesha kupokea zawadi kochokocho kutoka kwa wahisani na mashirika. Mimi humpamba punda wangu vizuri na ukimuona utadhani ni binti mrembo. Tunashauriwa kumtunza punda ili atutunze. Hilo nimelidhihirisha mwenyewe kwani urafiki nilio nao na punda wangu umewasukuma watalii kutaka kumpanda punda huyo, hivyo napata fedha,” akasema Bw Abbas.
Kwa wengine wao, msimu wa siasa umeanza kuwaletea baraka kwani wanalipwa kuvisha punda wao nembo za wanasiasa mbalimbali.
Bw Yusuf Hamza anasema ni kupitia mbinu ya kuwapamba punda wao ambapo wanasiasa wametambua wanaweza kukodisha punda kupiga kampeni, hasa wakati wa mikutano ya hadhara na wanapofanya misafara mjini Lamu.
Wamiliki wa punda ambao wamewarembesha mjini Lamu wakisubiri kutuzwa wakati wa mashindano ya siku ya kitaifa ya kulinda maslahi na haki za punda mwaka 2021. PICHA | KALUME KAZUNGU