Usafiri sasa si jinsi ulivyozoeleka Mombasa ‘2/2/22’ ikianza
NA WINNIE ATIENO
MAAFISA wa trafiki mjini Mombasa, leo Jumatano wanatarajiwa kuwa na kibarua kigumu kuelekeza magari katika mkondo mpya wa barabara za kisiwani baada ya serikali ya kaunti hiyo kufanya mabadiliko makubwa.
Maafisa wa kaunti hiyo wamekiri kuwa huenda mpango huo uliobandikwa jina 2/2/22 ukatatiza uchukuzi unapoanza kutekelezwa.
Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Miundomsingi katika kaunti hiyo, Bw Tawfiq Balala, alisema mfumo mwingine uliokuwa umezinduliwa awali ulio maarufu kama Happy Hour, sasa umefutiliwa mbali.
Katika mkondo huo ambao Gavana Hassan Joho alianza kuvumisha wiki iliyopita, baadhi ya barabara zitageuzwa kuwa za magari yanayoelekea upande mmoja pekee.
Mpango huo unatarajiwa kuanza kutumiwa kuanzia leo saa kumi na moja asubuhi kisiwani.
Barabara ambazo zitaathirika ni kama vile Digo Road, Ronald Ngala, Jomo Kenyatta na Sheikh Abdalla Farsi.
“Tunachomaanisha ni kwamba, unapoingia kisiwani kutoka Daraja la Nyali, magari yote yatatakikana kuelekea upande wa kushoto ili kuingia barabara ya Sheikh Abdalla Farsi badala ya kwenda moja kwa moja kuelekea Saba Saba. Hakuna tena kwenda moja kwa moja kuelekea Saba Saba,” akaeleza.
Kwa msingi huo, pande zote mbili za barabara eneo la Buxton zitatumiwa na magari yanayoingia mjini.Magari yataelekea hivyo hadi katika mzunguko wa Barclays eneo la Bondeni, ambapo yatachukua njia ya kuelekea Saba Saba na kurudi hadi barabara kuu ya Mombasa-Malindi.
Majaribio yamepangiwa kufanywa kwa siku 10.
Malori yanayozidi tani 10 yatapigwa marufuku kuingia katikati mwa jiji kuanzia saa kumi na moja asubuhi hadi saa mbili jioni. Yatatakikana kutumia maeneo ya Shimanzi na Mbaraki pekee katika saa hizo.
“Happy Hour ilikuwa ni mpango wa muda, lakini huu mpango mpya tunaozindua utakuwa wa kudumu ili kutatua misongamano. Natarajia kutakuwa na matatizo katika wiki za kwanza kwa sababu ni mwanzo mpya. Madereva wengi watajikuta upande mbaya wa barabara lakini kuna maafisa wetu wa trafiki pamoja na polisi katika kila makutano ya barabara kutoa usaidizi,” akasema Bw Balala.
Mkuu wa polisi wa trafiki eneo la Pwani, Bw Peter Maina, alisema baada ya siku tatu utathmini utafanywa kubainisha kama kuna chochote kitakachohitaji kubadilishwa.
Mratibu wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, Bw Salim Mbarak, na Mkurugenzi wa Chama cha Wachukuzi Kenya, Bw Ahmed Juneja, walikosoa mpango huo na kusema haukushirikisha umma kamwe.
Next article
Kamishna mpya ataka matumizi bora ya mali ya umma