WANTO WARUI: Uteuzi wa wanafunzi katika shule za upili ulikiuka haki za wengine
NA WANTO WARUI
WIKI jana, Wizara ya Elimu iliwateua wanafunzi waliofanya mtihani wa Darasa la Nane, KCPE, shule ambazo watajiunga nazo katika Kidato cha Kwanza baadaye mwezi ujao wa Mei.
Wanafunzi hao wapatao milioni 1.2 walipata habari kupitia rununu baada ya matokeo hayo kutangazwa.
Kila mmoja wao alikuwa na matumaini makubwa ya kujiunga na shule inayoambatana na uwezo wake wa kimasomo.
Hata hivyo, hali haikuwa hali tena baada ya baadhi ya wanafunzi walioweza kujipatia zaidi ya alama 400 kukosa shule za kitaifa.
Kulingana na Waziri wa Elimu George Magoha, wanafunzi waliopata alama 400 katika mtihani huo walikuwa 11,857.
Baada ya uteuzi huo wa shule, wanafunzi wapatao zaidi ya 38,000 walipata mialiko katika shule za kitaifa.
Hivi ni kusema kuwa, kuna zaidi ya wanafunzi 26,000 ambao hawakufikisha alama 400 na waliteuliwa kujiunga na shule za kitaifa.
Bila shaka, huu ni udhalimu kwa mwanafunzi aliyepata alama 400 kukosa shule ya kitaifa huku wanafunzi zaidi ya 26,000 aliowashinda wakijivunia nafasi hizo.
Kwamba, wanafunzi waliosomea katika mazingira magumu na kufanya vyema walihitaji kupata nafasi za shule za kitaifa haimanishi kuwa, wale waliopata alama 400 wakose nafasi katika shule hizo maadam hata idadi yao haikuwa kubwa.
Jambo la msingi, ambalo Wizara ya Elimu ilistahili kufanya ni kuwapa wanafunzi wote 11,857 waliopata alama 400 nafasi katika shule za kitaifa kisha nafasi zilizobaki ambazo ni zaidi ya 26,000 zigawiwe hao wengine, wakiwemo wale waliofanyia mtihani katika mazingira magumu.
Mara nyingi serikali imekariri kuwa Wanaofanya uteuzi huu wanafaa kuwajibika na kutenda kazi ifaavyo ili kudumisha amani na mshikamano nchini.
Ukandamizaji wa wanafunzi unaweza kulilitea taifa matatizo siku za baadaye.