‘Vifaranga’ wa Joho sasa kujitetea kivyao
PHILIP MUYANGA Na WINNIE ATIENO
WANASIASA katika Kaunti ya Mombasa, ambao nyota yao iling’aa waliposhirikiana na Gavana Hassan Joho kupiga kampeni 2017, sasa wamelazimika kujipanga upya bila mchango uliotokana na umaarufu wa gavana huyo.
Miongoni mwao ni wabunge Mishi Mboko (Likoni), Abdulswamad Nassir (Mvita), Badi Twalib (Jomvu), Asha Mohamed (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake), Seneta Mohammed Faki na baadhi ya madiwani.
Kwa miezi kadha sasa, wanasiasa hao wamekuwa wakishirikiana kuandaa mikutano ya hadhara ya kisiasa.Kulingana na Bi Mboko, gavana huyo alichangia pakubwa katika kuwasaidia wengi wao kushinda nyadhifa za kisiasa.
Ikizingatiwa kuwa Bw Joho amekaribia kumalizia kipindi chake cha ugavana, Bi Mboko alikiri kuwa imebidi wanasiasa wapange mikakati yao upya.“Sisi ni wanafunzi wa kisiasa wa Gavana Joho. Mimi na Bw Nassir ni wa timu ya Joho,” alisema Bi Mboko.
Mbuge huyo alifichua kuwa safari yake ya kisiasa imekuwa bora kutokana na msaada wa kisiasa wa Bw Joho na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.Kwa upande wake, Bw Nassir anasema kikosi cha wanasiasa wa ODM katika Kaunti ya Mombasa kimekomaa vya kutosha,kiasi cha kukiwezesha kuzoa viti vingi uchaguzini ikiwemo kiti cha ugavana.
Huku akionekana kumlenga Naibu Rais William Ruto na kikundi chake cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Nassir asema wasidhani ngome hiyo ya kisiasa ya Bw Odinga sasa imebaki bila nahodha.“Hii leo unapotazama, Raila hayuko hapa na wala Joho hayuko hapa.
Huu ni mkutano ambao umeandaliwa na watoto wao, wakiwemo Bi Mboko, Bw Faki na Ashu,” alisema Bw Nassir katika mojawapo ya mikutano iliyovutia umati mkubwa katika eneobunge la Likoni.
Wanasiasa hao waliamua watampigia debe Bw Nassir kuchukua usukani wa ugavana baada ya Bw Joho kufunganya virago mwaka ujao.Kulingana na wadadisi wa siasa, hatua hii ya kuunga mkono mmoja wao kuwania ugavana ni mojawapo ya mbinu wanazolenga kutumia wanasiasa hao ili kulinda mwelekeo wa siasa zao baada ya Bw Joho kung’atuka mamlakani.
Mchanganuzi wa masuala ya siasa, Prof Hassan Mwakimako asema hatua ya wanasiasa hao kuamua kujitegemea ni mwelekeo mzuri, kwani kuna uwezekano mkubwa umaarufu wa Bw Joho utashuka asipowania kiti chochote cha kisiasa.
Prof Mwakimako alisema kuwa wanasiasa hao wana nafasi bora zaidi kusikizwa na wananchi iwapo watasimama kivyao bila kuonekana wanamtegemea gavana huyo anayeondoka.Kauli sawa na hii ilitolewa na mchanganuzi mwingine, Prof Halimu Shauri.Kulingana naye, magavana wanaong’atuka uongozini wanaweza kuwa na ushawishi tu kwa kundi dogo la wapigakura ambao pengine walifaidi kutokana uongozi wao kibinafsi.
“Kusema kweli, wananchi wengi hawajafaidi kutokana na uongozi wa magavana, na hivyo basi itakuwa vigumu kwa gavana anayestaafu kushawishi siasa katika uchaguzi ujao,” akasema Prof Shauri.Hata hivyo, mchanganuzi wa kisiasa, Bw Herman Manyora, alitofautiana na kauli hizo akisema hata kama magavana wanaondoka, waliwekeza pakubwa kujenga sifa zao za kisiasa na rasilimali, ambazo bado wanaweza kutumia kushawishi umaarufu wa wanasiasa wengine.
Kulingana naye, haitakuwa jambo la kushangaza iwapo kwa mfano kuna magavana wanaoondoka wanaotaka kuhakikisha atakayerithi kiti cha ugavana ni mwandani wao anayeweza kuendeleza miradi yao.
Next article
Ngilu atoa hakikisho kortini kuwa atalipa madaktari…