Vijana 200 wa Thika wakamilisha kozi za kuwafaa maishani
Na LAWRENCE ONGARO
VIJANA mjini Thika, wamehimizwa kujihusisha na kozi zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Mnamo Jumanne, vijana wapatao 200 walipokea vyeti vyao vya kuthibitisha kufuzu kazi ya udereva.
Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina aliwafadhili vijana hao kuhudhuria mafunzo ya udereva kwa mwezi mmoja kupitia fedha za hazina ya maendeleo NG-CDF.
Vijana hao baada ya kufuzu kuwa madereva wamepokea leseni zao ambapo wataweza kupata ajira kutokana na ujuzi wao wa udereva.
Mbunge huyo alieleza kuwa ataendelea kuchukua hatua hiyo ya kuwafadhili vijana kuhudhuria kozi ya udereva na kazi nyingine muhimu.
“Ninaelewa vijana wakihamasishwa umuhimu wa kupata kozi fulani bila shaka hakuna yeyote atakayehangaika,” alifafanua mbunge huyo.
Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina (mwenye kofia) akiwa na baadhi ya vijana walionufaika na kozi za kuwafaa maishani. PICHA | LAWRENCE ONGARO
Vijana wengi waliohojiwa kuhusu hatua iliyochukuliwa na mbunge huyo, walisema ya kwamba hiyo ni njia moja ya kuwafunza vijana hao jinsi ya kutega samaki badala ya kupewa kila mara kutoka kwa wazazi ama mtu yeyote yule.
Vijana hao pia walihimizwa kuwa mstari wa mbele kuzingatia kozi tofauti ili kila mmoja aweze kujitegemea vilivyo katika maisha yake.
“Hatungetaka kuona vijana baada ya kukamilisha masomo yao wanaonekana tena wakitafuta ajira bila mafanikio,” alieleza Bw Wainaina.
Alisema asilimia kubwa ya vijana ndio hawana ajira na kwa hivyo ni muhimu kuwatafutia mahali pa kupata ajira badala ya wao kungoja eti wataajiriwa na serikali.
Vijana waliopokea mafunzo ya udereva walipongeza juhudi za mbunge wao kuwajali na kuwapa mwelekeo wa kimaisha.