Connect with us

General News

Viongozi wa kidini watumie fursa hii kuhubiri amani nchini – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Viongozi wa kidini watumie fursa hii kuhubiri amani nchini – Taifa Leo

TAHARIRI: Viongozi wa kidini watumie fursa hii kuhubiri amani nchini

NA KITENGO CHA UHARIRI

HUKU ikisalia miezi minane kabla ya Wakenya kuelekea debeni kuwachagua viongozi wapya, joto la kisiasa linatarajiwa kupanda nchini.

Hii ni kwa sababu wanasiasa wanaogombea viti vyote sita katika uchaguzi huo wa Agosti 9, wanatarajiwa kuendeleza kampeni zao.

Kwa hivyo, wanasiasa hao ndio wahusika wakuu katika mchakato huo. Hivyo basi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wamedumisha amani wanaposhindania kura za Wakenya.

Hii ndiyo maana tunaunga mkono ushauri ambao viongozi wa kidini walitoa kwa wanasiasa kwamba wakome kutumia lugha ya kuchochea chuki na fujo wanaposaka kura za raia.

Wakiongea na wanahabari baada ya kuongoza ibada za kukaribisha mwaka mpya, kiongozi wa kanisa la Kianglikana nchini (ACK) Askofu Mkuu, Jackson Ole Sapit na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nyeri, Antony Muheria, waliwataka wanasiasa kushindania viti kwa njia ya heshima isiyoleta fujo na vita.

Miito hii ina mashiko ikizingatiwa kuwa taifa hili limewahi kuathirika pakubwa na ghasia zilizoshuhudiwa kabla na baada ya chaguzi za 2007, 2013 na 2017.

Wananchi wa kawaida, hasa akina mama, watoto na wakongwe ndio walioathirika zaidi katika fujo hizo za kisiasa, zilizochochewa kwa kiwango kikubwa na matamshi ya wanasiasa.

Uchumi wa nchi nao umekuwa ukipata pigo nyakati kama hizo, baada ya wawekezaji kutoroka wakihofia hasara.

Hali hii huathiri raia hasa wa mapato ya chini, wala si viongozi matajiri.Hii ndiyo maana mwaka huu, wanasiasa wanapaswa kudhibiti ndimi zao wanapoomba kura ili pasitokee rabsha zozote zitakazoathiri uchumi ambao umeathiriwa na janga la Covid-19.

Lakini wajibu wa kuhubiri amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu ujao haupaswi kuchukuliwa kama wa wanasiasa pekee.

Askofu Ole Sapit, na wenzake, pia wanafaa kuhubiri amani katika makanisa yao na maeneo mengine ya kuabudu.

Hii ni kwa sababu asilimia kubwa ya wapigakura nchini ambao watashiriki katika uchaguzi mkuu ujao ni waumini katika makanisa makubwa nchini kama vile ACK na kanisa Katoliki.

Kwa hivyo, mbali na kutoa wito kwa wanasiasa kudumisha amani wanapoendesha kampeni zao, viongozi wa makanisa haya, na mengine, pia wawashauri waumini wao kukoma kuchochewa na wanasiasa. Sawa na wanasiasa, viongozi wa kidini wana ushawishi mkubwa zaidi kwa wananchi.

Ni wakati kama huu ambapo wanahitajika kutumia ushawishi wao kwa ajili ya kulinda “kondoo” wao wasipotoshwe na wanasiasa.