Connect with us

General News

Viongozi wahama UDA sababu ya ghasia – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Viongozi wahama UDA sababu ya ghasia – Taifa Leo

Viongozi wahama UDA sababu ya ghasia

Na WINNIE ATIENO

BAADHI ya viongozi waliokuwa wakilenga kutafuta tikiti ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuwania viti mbalimbali vya kisiasa Mombasa mwaka ujao, wameamua kuhama chama hicho wakilalamikia ghasia chamani.

Wanasiasa hao waliamua hivyo kufuatia kisa ambapo mshirikishi wa UDA eneo la Pwani, Bw Mohammed Tenge, alicharazwa kama mbwa na watu wanaodaiwa walitumwa na baadhi ya wanasiasa ambao ni wandani wa naibu rais eneo hilo.

Mwaniaji wa kiti cha useneta katika chama cha UDA Bw Abdulsalaam Kassim alitangaza kuhama chama hicho kufuatia ghasia hizo.

“Nimeshangaa kwa nini hakuna hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa na wakuu wa chama. Hata hivyo nimehama UDA na nitakuwa mgombeaji huru nikipigania useneta hapa Mombasa,” alisema.

Mwenzake anayepigania Ugavana Bw Mohammed Bahaidar naye alihama chama hicho na kukashifu uongozi wake kwa kutowachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa ghasia hizo.

Vile vile, walilalamika kuwa chama kimetekwa na watu wachache ambao wanataka kudhibiti shughuli zote na hivyo inahofiwa hakutakuwa na mchujo kwa njia ya haki kuelekea kwa uchaguzi ujao.

Bw Tenge alimuonya Naibu wa Rais kuwa mwangalifu akidai kuwa baadhi ya wanasiasa waliomzingira si waaminifu wanavyomtaka kuamini.

Bw Tenge na Dkt Sanjeev Agarwal ambaye alitaka tikiti ya UDA kuwania ugavana wa Mombasa walishambuliwa wakapigwa Jumamosi walipokuwa katika msafara wa Dkt Ruto, punde alipokuwa amewasili Mombasa kwa maandalizi ya kuanza rasmi kampeni zake.

Akiongea nyumbani kwake eneo la Sega, Kaunti ya Mombasa anakoendelea kuuguza majeraha, Bw Tenge alisema tayari amepiga ripoti kwa polisi na anataka haki itendeke.

“Nilipigwa kidogo nife. Nimepiga ripoti katika kituo cha polisi cha Nyali na ninairai idara ya usalama ichunguze ghasia hii ambayo isipochukuliwa maanani huenda ikazua balaa wakati wa uchaguzi mkuu hapo mwakani. Nimeenda hospitali na kutibiwa lakini bado nina maumivu,” alisema Bw Tenge.

Kulingana na wadakuzi wa Taifa Leo, kizazaa kilianza wakati Dkt Agarwal alijaribu kumpokea Naibu wa Rais katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi huko Mombasa na baadaye katika jumba lililo Nyali kabla ya kuzuiliwa na wandani wa wanasiasa wengine wa UDA.

Bw Tenge alisema alipigwa na vijana ambao walitumia silaha butu na kumng’oa jino.

“Nilipoteza pesa zangu kwenye ghasia hizo. Naibu wa Rais hajanijulia hali, ni Farouk Kibet (msaidizi wake) pekee. Chama kimeanza kuingia doa sababu ya tamaa ya baadhi ya viongozi wanaojiona wako karibu na Dkt Ruto.

“Hao ni watapeli wanakudanganya ndugu yangu. Mimi nilijitolea mhanga na kufa na chama sitahama hata waniuwe,” alisema hapo jana nyumbani mwake anakoendelea kuuguza majeraha. Ripoti ya hospitali ya Jocham ambako Bw Tenge alikimbizwa kwa matibabu inaonyesha alipata majeraha usoni, mgongo, tumbo na kungo’olewa jino.

Alimtaka kiongozi wao wa chama kuingilia kati suala hilo.

“Dkt Ruto ondoa ghasia katika chama, usikubali watu wachache ambao wanatumiwa na wanasiasa wengine kuharibu UDA,” alisema Bw Tenge.

Dkt Ruto alianza ziara zake Pwani wikendi ambapo alifanya mikutano kadhaa Kaunti ya Mombasa, kabla kuelekea Kilifi baadaye jana.

Lalama hizo zinatishia kutia doa UDA ambapo viongozi wake wamekuwa wakipigia debe chama hicho kama cha kuleta umoja na amani kwa wananchi, wakidai kuwa tofauti na vyama vingine ambavyo wanavihusisha na ghasia.

Dkt Ruto aliandamana na wabunge Aisha Jumwa (Malindi) Kiman Ichungwa(Kikuyu), Kimani Ngunjiri (Bahati), Mohamed Ali, (Nyali), Benjamin Tayari (Kinango) na aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar, ambaye pia anawania kiti cha ugavana wa kaunti hiyo kupitia chama cha UDA.