Vita vya ubabe vyazuka ndani ya Azimio la Umoja
NA WAANDISHI WETU
MGAWANYIKO umeibuka miongoni mwa wandani wa kinara wa ODM Raila Odinga ambaye yuko ziarani nchini India kuhusu usimamizi wa kampeni za Azimio La Umoja.
Mpasuko huo huenda ukatatiza kampeni za urais za waziri mkuu huyo wa zamani kupitia muungano wa Azimio la Umoja.
Baadhi ya viongozi kutoka Nyanza na Magharibi wanahisi kupuuzwa baada ya kikosi kinachoongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Sabina Chege na mbunge wa Kieni Kanini Kega kutwikwa jukumu la kuzunguka maeneo hayo kumpigia debe Bw Odinga.
Viongozi wa ODM wakiongozwa na magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Wilbur Ottichil – lo wa Vihiga hawakujitokeza kwenye mikutano iliyoandaliwa na kikosi cha Bw Joho katika kaunti zao.
Mpasuko miongoni mwa wandani wa Bw Odinga ulijitokeza wazi wiki iliyopita ambapo kikosi cha Bw Joho kiliongoza mkutano wa Azimio la Umoja katika eneo la Magharibi.
Bw Joho na wenzake walihutubia mkutano wa kisiasa katika Kaunti ya Vihiga Alhamisi wiki iliyopita na kisha kuelekea Busia siku iliyofuatia.
Kabla ya kuelekea Magharibi, kikosi cha Bw Joho kilifanya mikutano katika maeneo ya Ugunja, Siaya, Bondo kwenye Kaunti ya Siaya.
Lakini Gavana Ottichilo na Bw Oparanya walisusia mikutano hiyo wakidai kuwa hawakushirikishwa katika mipango.
Bw Ottichilo hakufurahishwa na hatua ya sekretariati ya Azimio kwa kupanga mkutano wa kisiasa katika kaunti yake bila kumshirikisha.
Katika mkutano wa Vihiga, Bw Joho alikuwa ameandamana na wabunge Chris Omulele (Luanda), Babu Owino (Embakasi Mashariki), Godfrey Osotsi (Maalumu), Junet Mohamed (Suna
Mashariki), Bw Kega, Gladys Wanga (Kaunti ya Homa) Bi Chege (Muranga) na Seneta wa Narok Ledama Ole Kina. Gavana Oparanya alisusia mkutano wa Busia na badala yake alihudhuria mazishi ya aliyekuwa mfuasi sugu wa AFC Leopards na Harambee Stars, Isaac Juma, kijijini Ebuyenjere, Mumias Magharibi, Kaunti ya Kakamega.
Inadaiwa kuwa Bw Oparanya alikerwa na hatua ya sekretariati ya Azimio kutuma Bw Joho kuongoza kampeni katika eneo hilo. Bw Oparanya aliongoza mkutano mwingine wa Azimio katika eneo la Busia wiki moja baada ya Bw Joho na kikosi chake kuondoka.
Lakini Bw Oparanya alijitetea kwa kusema alikosa kuhudhuria mkutano wa Azimio katika Kaunti ya Busia kwa sababu alikuwa kwenye mkutano mwingine wa bodi ya kampeni za Bw Odinga uliodumu kwa takribani masaa sita.
“Kiongozi wa chama (Raila) anapokuwa nje ya nchi, mimi hujitwika jukumu la kuhakikisha kuwa mipango ya kampeni zake inaendelea. Madai kwamba nalenga kujiunga na United Democratic Alliance (UDA) hayana mashiko,” akasema Bw Oparanya.
Katika eneo la Nyanza, wanasiasa wakiongozwa na mbunge wa Suba Kusini John Mbadi na mwenzake wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo wameshutumu Bi Wanga kwa kutumia mkutano wanaodai kuwa wa Azimio la Umoja kuzindua kampeni zake za ugavana, Jumapili.
Ripoti ya Rushdie Oudia, Benson Amadala na George Odiwuor