Vituko vilivyoshuhudiwa wakati wa ibada ya kumuaga Kibaki
NA WANGU KANURI
IBADA ya wafu ya kumuaga aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya, Emilio Mwai Kibaki iliwajumuisha Wakenya, viongozi wa Kenya pamoja na mataifa mengine.
Hata hivyo, ibada hiyo haikukosa vioja vyake.
Walinzi wa Raila Odinga walizuiliwa kuingia katika eneo la watu mashuhuri.
Raila ambaye alikuwa ameandamana na mke wake Ida Odinga waliruhusiwa kuingia peke yao huku walinzi wao wakikatazwa.
Mlinzi mmoja aliyekuwa amevalia suti yenye rangi ya kijivu alijaribu kuingia kwa nguvu lakini akakamatwa na kukatazwa.
“Usilete fujo hapa,” afisa mmoja akamfokea.
Inadaiwa kuwa maafisa waliowakataza walinzi wa Raila walikuwa wamepewa masharti ya kuwaruhusu tu watu mashuhuri bila ya walinzi wao.
Kwa upande mwingine, Rais Uhuru Kenyatta alikwepa kumsalimia naibu wake William Ruto walipokuwa kwenye uwanja wa Nyayo. Ruto aliinama na kuonyeshana ishara ya mikono huku Kenyatta akikunja ngumi na kuweka mikono yake nyuma.
Kutosalimiana kwao kulishuhudiwa tena mapema wiki hii wakati Kenyatta alifika bungeni ili kuwaongoza Wakenya katika kutazama mwili wa marehemu Kibaki lakini hawakusalimiana kwa mikono.
Wawili hao ambao walionekana kwa mara ya kwanza Jumatatu tangu Desemba 12, 2021 wamekuwa maadui wa kisiasa licha ya kuwa wandani wa karibu hapo zamani.
Uadui wao unatokana na Rais Kenyatta kutangaza kuwa atamuunga Raila kuwa mrithi wake hatua inayoenda kinyume na ahadi aliyoitoa walipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2013.
Hali kadhalika, Wakenya waliokuwa waking’ang’ania miavuli iliyokuwa ikipatianwa nje ya uwanja wa Nyayo walipoteza simu zao.
Kina mama hao ambao waligundua simu zao zilikuwa zimeibiwa waliwaomba wenzao wawapigie huku wakizitafuta mifukoni mwa nguo walizokuwa wamevalia.
“Simu imeenda hebu nipigie,” wakasikika wakisema.
Ibada ilipokuwa ikitamatika, mwanamume mmoja alifika kwenye jukwaa na kumuomba padre dakika chache aweze kutoa rambirambi zake.
“Nipe tu dakika mbili niweze kutoa rambirambi zangu,” akasema kabla hajaondolewa na walinzi.
Mapema wiki hii, mwanamume yuyo huyo anayedai kuwa na ukaribu na Rais Kibaki alisababisha sarakasi bungeni baada ya kupiga mayowe alipokuwa akimwomboleza mwendazake.
“Mbona umeenda haraka hivyo?” akasema huku akitokwa na machozi.
Licha ya juhudi za kumliwaza kugonga mwamba, polisi walimwondoa mwanamume huyo bungeni ambaye kwa wakati huo alikuwa ashavua nguo zake huku akiomba kuona mwili wa ‘babu’ yake.