PENGINE tayari unajua kuwa tunda aina ya tufaha ni bora maradufu kuliko kipande cha chokoleti ambayo imejazwa sukari.
Huo ni uelewa wa kawaida tu, na kwa baadhi ya watu wanaojali afya zao, ufahamu kama huo huwafanya wakazingatia ulaji unaoshauriwa kiafya.
Lakini pia, kuna baadhi ya wale ambao wanalenga kuchukua hatua zaidi katika kuzingatia misingi bora ya afya zao.
Kwa baadhi ya vyakula, kuvichemsha, kuvipika, kuoka, kuchoma na aina nyingine ya upishi hufanya vikaongeza kiwango cha virutubisho na hivyo ukila mwili wako huongeza mahitaji muhimu ili kuwa wenye afya zaidi.
Lakini pia, kuna baadhi ya vyakula ambavyo ukipika vinapunguza kiwango cha virutubisho ilivyonavyo ukilinganisha na ikiwa ungekula vyakula hivyo vikiwa vibichi.
Ingawa baadhi ya vyakula huwa na ladha nzuri vinapokuwa vimepikwa, lakini yawezekana kabisa kuwa kwa kuvipika umepata ladha lakini ukapoteza virutubisho muhimu kwa afya yako.
Kiazisukari (Beet root)
Kiazisukari cha rangi nyekundu kinaweza kuwa aina ya mbogamboga yenye sukari kwa kiasi kikubwa, lakini manufaa yake ni makubwa zaidi kwa sababu huwa na virutubisho muhimu.
Viazisukari vina kiwango kikubwa cha vitamini C, nyuzinyuzi, potassium, manganese, na vitamini B folate ambayo huwa na faida nyingi za kiafya zinazoweza kuimarisha kinga yako ya mwili, kukuboresha na kupunguza shinikizo la damu.
Inaweza kukuchukua muda kuzoea ulaji wa kiazisukari kikiwa kibichi, kwa hiyo ikiwa utaamua kula, basi changanya hata na kachumbari yenye karoti, matufaa, tangawizi na limao.
Brocolli
Brocolli ni aina ya mboga ambayo kwa umuhimu wake ina kiwango kikubwa cha faida za kiafya, mboga hii si tu kwamba ina kiwango kikubwa cha vitamini C, bali pia ina calcium, potassium na protini.
Vilevile, brocolli hupunguza shinikizo la damu, huboresha afya ya moyo, na pia huwa na madini yanayosaidia kukabiliana na kuzeeka na kuongeza kinga ya mwili.
Ikiwa inakuwia vigumu kula mbichi kama ilivyo, jaribu kutengeneza supu ya brocolli mbichi ili upate ladha zaidi.
Vitunguu maji
Vitunguu maji husaidia kuboresha afya ya mishipa na moyo, na kupunguza shinikizo la damu.
Kula kitunguu kibichi kutakusaidia kukabiliana na virusi wanaosababisha magonjwa kama kikohozi na mafua.
Pilipili mboga
Pilipili mboga (hasa nyekundu) hupaswa kuwepo kwenye mpangilio wako wa chakula. Zikiwa na zaidi ya mara tatu ya kiwango cha vitamini C unachohitaji kwa siku, pilipili mboga pia hufahamika kuwa na anti-oxidants na ni chanzo kikubwa cha vitamini B6, vitamini E na magnesium.
Pilipili mboga za kijani kibichi. PICHA | MARGARET MAINA
Inawezekana kupika au kuoka pilipili mboga lakini kwa kufanya hivyo, husababisha kiwango kikubwa cha vitamini C kuondoka. Kwa kula zikiwa mbichi hata kwa kuchanganya kwenye kachumbari yako kuna faida kiafya.
Kitunguu saumu, nazi na njugu pia ni muhimu kuliwa mbichi.