KAMAU: Vyuo vikuu nchini viige vile vya bara Ulaya na Amerika
Na WANDERI KAMAU
SIMULIZI kuhusu ‘kuanguka’ kwa Chuo Kikuu cha Moi, mjini Eldoret, ni chungu.
Ni simulizi inayofanana na wasifu wa mtu aliyefariki.
Ni simulizi ya kusikitisha, kufadhaisha na kuatua moyo.
Kwanza, chuo hicho ni miongoni mwa taasisi za elimu ya juu ambazo zinasifika sana nchini kutokana na ubora wa mafunzo kinayotoa.
Ndicho chuo cha pili kubuniwa nchini, baada ya Chuo Kikuu cha Nairobi.
Hivyo, ni taasisi ambayo imechangia sana katika ustawi wa elimu nchini, barani Afrika na duniani kote.Watu waliosomea chuoni humo wanasifika kote duniani kutokana na utaalamu wao wa hali ya juu.
Hivyo, ripoti kwamba chuo hicho kitalazimika kuongeza karo ili kushughulikia masuala yake ya msingi, ni pigo kubwa kwa ustawi na ukuaji wa sekta ya elimu nchini.
Kulingana na Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, zigo kuu linaloandama chuo hicho ni deni la zaidi ya Sh4.5 bilioni.
Vile vile, kinaandamwa na laana ya ukabila: kama vyuo vikuu vingine nchini, pia hicho kinadaiwa kuwapendelea watu wa jamii fulani kwenye taratibu za kuwaajiri wafanyakazi.
Katika enzi hii ya karne ya 21, ambapo dunia inategemea taasisi za elimu ya juu kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoiandama, ni sikitiko ikiwa taasisi hizo haziwezi kujisimamia kifedha bila kusaidiwa ama kufadhiliwa na serikali.
Katika nchi zilizostawi kiuchumi duniani kama Amerika na Uingereza, ni vigumu sana kusikia taasisi muhimu kama chuo kikuu ikianguka ama kufilisika kwa sababu ya usimamizi mbaya.
Vyuo hivyo pia huwa na utegemezi mdogo sana kutoka kwa serikali.
Nchini Amerika, vyuo vikuu kama Harvard au Washington State University huwa taasisi huru, ambazo wakati mwingine huisaidia serikali ya Amerika kufadhili baadhi ya shughuli za utafiti.
Vyuo hivyo pia huwa washirika wa karibu wa serikali katika kutafuta suluhisho kwa matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kisayansi yanayoyakumba mataifa hayo.
Kwa mfano, chanjo dhidi ya virusi vya corona ilipatikana kupitia ushirikiano ulioendeshwa na vyuo vikuu pamoja na taasisi kadhaa za kisayansi.
Pasingekuwapo na ushirikiano huo, pengine dunia ingekuwa inaendelea kuzongwa na makali ya corona.
Bila shaka, uhalisia huo unapaswa kuwa changamoto kwa taasisi za elimu ya juu hapa nchini, ili zibuni njia za kujisimamia na kujikuza bila kutegemea msaada wa serikali.
[email protected]