[ad_1]
Wachina 8 taabani kwa kufanya kazi bila vyeti vya serikali
Na RICHARD MUNGUTI
RAIA wanane kutoka Uchina Ijumaa walitozwa faini ya Sh400,000 kwa kufanya kazi nchini bila vyeti kutoka Idara ya Uhamiaji.
Kila mmoja aliagizwa alipe faini ya Sh50,000 ama atumikie kifungo cha miezi sita gerezani.
Washtakiwa hao Xie Liguang , Zhang Liyi,Cong Tingting, Qiao Liuping, Zhang Jie, Zhang Tili, Long Yujie na Liu Rong walifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Wendy Kagendo Michemi.
Walikiri shtaka kupitia kwa mkalimani Samuel Omondi. Shtaka dhidi ya wanane hao lilisema mnamo January 14 katika jengo la Ur Home International Kenya Limited kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa kaunti ya Nairobi walipatikana wakifanya kazi bila cheti kutoka idara ya Uhamiaji.
Shtaka lilisema washtakiwa hao walikuwa wakiuza dari na vigae vya sakafu.
Kiongozi wa mashtaka Bw Alexander Gikunda alieleza mahakama kwamba maafisa kutoka idara ya uchunguzi wa jina (DCI) walifahamishwa kwamba kulikuwa na raia wa kigeni waliokuwa wanafanyakazi nchini bila idhini.
“Maafisa kutoka DCI walitembelea afisi za kampuni ya Ur Home International iliyoko barabara kuu ya Mombasa-Nairobi na kuwapata washtakiwa wakifanya kazi bila vyeti kutoka idara ya uhamiaji,” Bw Gikunda alisema.
Hakimu alifahamishwa washtakiwa hao walikamatwa na kuzuiliwa. Hata hivyo mnamo Januari 17, washtakiwa hao kupitia ubalozi wao waliwasilisha maombi katika Idara ya Uhamiaji ya kupewa vibali vya muda vya kufanya kazi nchini.
“Idara ya Uhamiaji iliwapa washtakiwa hawa vibali vya kufanya kazi nchini kwa muda wa miezi minne,” Bw Gikunda alisema.
Vibali hivyo vilikabidhiwa hakimu. Hata hivyo , Bw Gikunda alisema washtakiwa walitiwa nguvuni kabla ya vyeti vya kuwahalalisha kuishi nchini wakifanya kazi.
[ad_2]
Source link