Connect with us

General News

Wadau waepushe raia kususia kura katika uchaguzi ujao wa Agosti 9 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wadau waepushe raia kususia kura katika uchaguzi ujao wa Agosti 9 – Taifa Leo

TAHARIRI: Wadau waepushe raia kususia kura katika uchaguzi ujao wa Agosti 9

NA MHARIRI

HUKU muda wa kujisajili kupiga kura ukikaribia kuisha, imeibuka kuwa wadau wakuu wanarushiana lawama kuhusu aliyekosa kuhamasisha umma kwa kiwango cha kutosha.

Katika miaka iliyopita ya uchaguzi hasa tangu mabadiliko yafanywe kwa tume ya uchaguzi baada ya uchaguzi wa 2007, wananchi walizoea hamasisho tele kuhusu hitaji la kujisajili kupiga kura.

Vile vile, kulikuwa na hamasa tele kuhusu umuhimu wa raia kushiriki katika uchaguzi kutoka kwa tume ya uchaguzi, wanasiasa na mashirika ya kijamii.

Mwaka huu hali imekuwa tofauti tangu wakati wa awamu ya kwanza ya usajili iliyoendeshwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Matarajio kwamba idadi ya wanaojisajili ingeongezeka siku za mwisho katika awamu ya kwanza yalizimwa kwani hilo halikutokea.

Dalili zaonyesha pia awamu hii haitakuwa kama zamani ambapo Wakenya waliendeleza desturi yao ya kusubiri hadi dakika za mwisho, ingawa kuna baadhi yetu ambao bado wana matumaini.

Baadhi ya maafisa wa IEBC, wanasiasa na viongozi wa kijamii wamelaumiana kila mmoja akidai kuwa mwenzake hakuweka mipango ya kutosha kuhamasisha umma.

Kwa upande wa IEBC, ni wazi kuwa kuna changamoto za kifedha kwani mwenyekiti Wafula Chebukati, amekuwa akilalamikia upungufu wa bajeti yao kwa muda mrefu sasa.

Huenda ikawa changamoto sawa na hii inakumba mashirika ya kijamii ambayo yamelegea sana katika miaka iliyopita, hasa baada ya kuekewa sheria kali za usimamizi punde baada ya Serikali ya Jubilee ilipoanza kushika uongozi wa taifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2013.

Hata hivyo, badala ya malalamishi haya, ni muhimu kwa wadau kuzingatia maoni ya wengine kuwa huenda ikawa wananchi hawaoni tena haja ya kushiriki katika mpango mzima wa kuchagua viongozi wao.

Imesemekana watu wengi wanapohojiwa kuhusu kama watajitokeza kupiga kura, wao husema huko ni kupoteza wakati kwa vile hawaoni manufaa yoyote kutoka kwa wanasiasa wanaochaguliwa mamlakani mara kwa mara.

Yale ambayo yameshuhudiwa wakati huu wa usajili huenda yakashuhudiwa tena wakati Uchaguzi Mkuu utakapofika. Hilo halitaonyesha picha nzuri kwa hatua kubwa ambazo nchi hii imepiga katika kukuza demokrasia.

Wadau wote wajihoji kuhusu mienendo hii inayoshuhudiwa baina ya wananchi, ili kuepusha hali ambapo idadi kubwa ya raia watakuwa wanaachia wachache jukumu zima la kuchagua viongozi siku za usoni.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending