Wafanyabiashara wapata hasara kufuatia marufuku ya vyuma chakavu
Na SAMMY KIMATU
WAFANYABIASHARA katika maeneo ya Viwandani, Kibera, Kariobangi na Mathare kaunti ya Nairobi wanakadiria hasara kubwa baada ya wateja wao waliowategemea kwa miaka mingi kufutwa kazi.
Hali hiyo imechangiwa na wafanyakazi katika viwanja vya kununua vyuma chakavu kukosa kazi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kufungwa kwa biashara ya vyuma vilivyotumika.
Miongoni wa walioathirika ni waendeshaji biashara za bucha, hoteli na vilabu.
Waliozungumza na Taifa Leo walisema wafanyakazi hao wamepiga jeki biashara zao kwa muda wa zaidi ya miaka 20 na sasa wanafikiria kufungasha virago kwa kukosa kazi.
“Kila asubuhi, zaidi ya watu 50 walikuwa wakinunua kifungua kinywa katika hoteli yangu na tangu waachishwe kazi, sina budi ila nifunge kioski changu,” mmiliki wa hoteli moja mtaani wa mabanda wa Lunga Lunga akasema.
Katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba, hali si tofauti kwani wafanyabiashara waliohudumia wateja kutoka yadi kadhaa za vyuma kuukuu nao wanalamika biashara imepungua maradufu.
“Kila siku, watu hao walikuwa wakipima kilo kadhaa za nyama ya mbuzi, nguruwe na ya ng’ombe huku jioni wakifurika katika baa wakimaliza kazi. Tangu rais Uhuru Kenyatta apige marufuku biashara ya vyuma kuukuu nchini, kazi imesambaratika,” mmiliki wa bucha katika steji ya Kayaba akanena.
Kwingineko, katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Shimo la Tewa na Mukuru-Kwa Reuben, maeneo ya kununua vyuma yalisalia kufungwa.
Katika mtaa wa mabanda wa Kibera Laini Saba, Line Nane, Mathare, Kariobangi na Gorogocho, maeneo ya biashara ya vyuma yalionekana kuwekwa kufuli.
“Ukiangalia hapa, hakuna wafanyakazi licha ya vyuma kurundikana hapa. Ni mimi pekee ndiye niko hapa kikazi,” mlinzi katika mtaa wa mabanda wa Kariobangi akansema kwa sharti asitambuliwe.
Katika mtaa wa Shimo La Tewa, zaidi ya mbwa kumi ndio walikuwa wamelala karibu na lango la yadi kubwa ya kununua vyuma.