Wafanyakazi wa serikali ya Kiambu wapata ajira ya kudumu
Na LAWRENCE ONGARO
WAFANYAKAZI wapatao 1,070 wa kaunti ya Kiambu, wamepata afueni baada ya maslahi yao ya kikazi kuchunguzwa na kutathminiwa.
Gavana wa kaunti hiyo Dkt James Nyoro , aliamuru wafanyakazi hao waajiriwe kupitia mkataba wa kudumu na marupurupu yao yaangaziwe vilivyo.
Gavana huyo alisema kwa muda mrefu wafanyakazi wengi wamekuwa wakifanya ajira za kibarua, bila kujivunia marupurupu ya kuwafaa.
“Ningetaka kuona mabadiliko katika wafanyikazi hao ili waweze kubadilisha hali yao ya maisha,” alifafanua gavana huyo.
Mwishoni mwa wiki jana, wafanyakazi hao walikongamana katika makazi makuu ya kaunti ya Kiambu ili kupokea habari njema kutoka kwa gavana huyo.
Mnamo siku ya siku, gavana aliwasilisha barua rasmi ya kuajiriwa kwao kwa mkataba wa kudumu, nao walionyesha furara tele nyusoni mwao.
Kulingana na mpangilio huo, wanawake wapatao 670 walipata nafasi ya kuajiriwa kwa mkataba wa kudumu huku wanaume 400 pia wakinufaika na mpango huo.
Baada ya kupokea barua hizo za ajira, wafanyakazi hao waliahidi kwamba wamejitolea kufanya kazi kwa bidii bila kulegea ili kaunti hiyo ya Kiambu iweze kuimarika zaidi.
“Ninawashauri nyinyi kama wafanyakazi wa kaunti hii mjikakamue ili kuinua kaunti yetu ili ifikie kiwango kingine,” alifafanua Bw Nyoro.
Alishangaa jinsi wafanyakazi wengi wamekuwa katika kiwango kimoja cha ajira kwa muda mrefu bila kupandishwa cheo jambo alilosema linaponza juhudi za wengi kuongeza bidii kazini.
Alisema wakati alipojiunga na kaunti hiyo mwaka wa 2020 hakukuwepo na mpangilio maalum kuhusu ajira ya wafanyakazi lakini kutokana na mipango yake alionelea kubadilisha hayo ili wafanyakazi wapige hatua katika maeneo wanayofanyia kazi yao.
Aliwahimiza wafanyakazi wasiyumbishwe na siasa zinazoendelea nchini, bali wajihusishe na kazi yao ili kuendesha Kaunti ya Kiambu mbele.