Wafanyikazi wanaopata mishahara duni wapewa nyongeza ya asilimia 12
NA WINNIE ONYANDO
RAIS Uhuru Kenyata ameagiza wafanyakazi wa ngazi ya chini waongezewe mshahara kwa asilimia 12.
Hii ilikuwa mara ya kwanza serikali kuongeza mishahara kwa watu wa chini katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Akizungumza Jumapili katika halfa ya kuadhimisha Leba Dei, Rais Kenyatta alisema kuwa hiyo ni njia ya kutambua juhudi na bidii ya wafanyakazi wanaoinua uchumi wa nchi na kuwawezesha kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha.
“Kwa kutambua mchango wa wafanyakazi wetu katika ujenzi wa uchumi na hali ngumu inayowakabili kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na janga la corona, na kutambua kwamba hawajaongezwa mishahara kwa miaka minne, ninatangaza nyongeza ya asilimia 12 ya mishahara ya kiwango cha chini,” alisema Rais Kenyatta.
Alisema wafanyakazi wataanza kufurahia nyongeza hiyo kuanzia mwisho wa mwezi huu.Rais aliwapongeza wafanyakazi nchini kwa ujasiri wao na hata kutambua juhudi walizofanya katika kuhakikisha kuwa nchi inajikwamua kutoka kwa athari za janga la corona.
Alisema kuwa serikali ilipunguza kodi zinazotozwa baadhi ya bidhaa nchini kama njia ya kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata vyakula na bidhaa muhimu kwa bei nafuu.
“Kujenga taifa sio tukio la siku moja ila ni mchakato wa pole pole. Unahitaji uvumilivu na ushirikiano. Baadhi ya nchi tunazoona ziking’aa zilijengwa kwa matumaini na uvumilivu,” akasema Rais Kenyatta.
Haya yanajiri huku Wakenya wakilalamikia gharama ya juu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa za kimsingi.
Bei za bidhaa kama vile sukari, gesi, mkate, maziwa, unga na petroli zimekuwa juu huku wengi wakishindwa kupata chakula cha kutosha.Bei ya unga imepanda kutoka Sh120 hadi Sh160 huku bei ya mkate na maziwa ikipanda kwa Sh10.
Bei ya mtungi wa kilo 6 wa gesi kwa sasa ni kati ya Sh1,500 na Sh1,800 kutoka Sh800 mwaka 2021.
Kumekuwa na uhaba wa petroli nchini, jambo lililofanya baadhi ya vituo vya petroli kufungwa na shughuli ya uchukuzi kukatizwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Rais alizionya kampuni za kuuza mafuta dhidi ya kusababisha uhaba ili kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi akisema watachukuliwa hatua.
“Kuna watu wanaouza mafuta nje ya nchi. Wanaona kuwa wakifanya hivyo watapata faida kubwa ikilinganishwa na wanayopata nchini. Tutawakomesha mara moja,” akasema Rais Kenyatta.
Alisema kuwa suala la mafuta ni nyeti na kuwa inahitaji ushirikiano ili kulitatua.
“Kuna viongozi wanaotoa ahadi hewa kwa Wananchi na kuwaelekeza kwangu kuutatua suala la uhaba wa petroli. Suala hilo si langu pekee bali inahitaji ushirikiano,” akasema