TAHARIRI: Wagombezi wenye sera nzuri ya spoti wachaguliwe
NA MHARIRI
HAIPINGIKI kwamba kati ya mambo yanayolikweza jina la Kenya katika medani ya kimataifa ni spoti hasa riadha.
Ingawa taifa hili liko katika nafasi nzuri kwenye chati ya michezo duniani, tunasadiki kuwa hatujafikia upeo wetu stahiki hasa katika mchezo wa kandanda.
Kwa hivyo, ni matumaini yetu kuwa wanasiasa wanaotaka viti mbalimbali kuanzia urais hadi kwa udiwani kwenye uchaguzi mkuu ujao, wataipa sera ya michezo umuhimu.
Wala yasiwe maneno matupu tu jinsi serikali ya Jubilee chini ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walivyofanya mnamo 2013 na 2017.
Wawili hao waliahidi makubwa kuhusu michezo hasa katika suala la miundomsingi mathalani viwanja vitano vya hadhi ya kimataifa na angaa akademia moja katika kila kaunti.
Ajabu ni kwamba kipindi cha viongozi hao wawili kinapokamilika, hakuna lolote la maana lililofanyika; hata uwanja mmoja tu wa kifahari haupo.
Hii ndiyo maana ni muhimu kwa wapigakura kuwachungua kwa dhati wawaniaji, hasa wa urais na ugavana watakaosisitiza makuzi ya michezo hasusan soka katika manifesto zao.
Ni kutokana na kasumba kuwa michezo ni tasnia ya burudani tu isiyohitaji uwekezaji wa maana, ndipo vijana wengi wenye vipawa “wanaozea” majumbani mwao kwa ufukara ilhali kwa sasa hasa katika mataifa ya bara Ulaya, michezo inachukuliwa kama sekta muhimu inayoweza kutoa fursa nyingi za kazi na hivyo basi kuwaajiri vijana wengi wanaohangaika na maisha bila jambo muhimu la kufanya linaloweza kuwaletea riziki.
Tungependa kumuona rais atakayeazimia kuisaidia timu ya taifa ya Kenya ya soka, Harambee Stars ifuzu kwa fainali za Kombe la Dunia la 2026 nchini Amerika, Mexico na Canada.
Kadhalika, itakuwa fahari kubwa kwa taifa hili kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika mwaka 2023 nchini Ivory Coast.
Wapo marais wanaojulikana waliojitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa timu zao za taifa wanazozipenda zimefuzu kwa vinyang’anyiro vikubwa kama vile fainali za soka za bara na zile za Dunia.
Sekta ya spoti inahitaji kutengewa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa cha bajeti ndipo zipate maandalizi mazuri na ya kisasa yanayohitajika katika ushindani wa hadhi ya juu.
Kwa kufanya hivyo, na kuzuia ufisadi, bila shaka yote yatawezekana, si katika soka tu bali katika fani nyinginezo zilizodumaa.