Connect with us

General News

Wagonjwa wateseka mgomo ukilemaza huduma zote za afya – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wagonjwa wateseka mgomo ukilemaza huduma zote za afya – Taifa Leo

Wagonjwa wateseka mgomo ukilemaza huduma zote za afya

NA SIAGO CECE

BAADHI ya wagonjwa katika Kaunti ya Kwale, wamelazimika kurudi makwao baada ya huduma zote kusitishwa katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Msambweni kutokana na mgomo wa wahudumu wa afya.

Uchunguzi wa Taifa Leo jana ulibainisha kuwa hospitali hiyo kubwa zaidi ya kaunti imebaki mahame huku mgomo wa wahudumu wa afya katika kaunti hiyo ukiingia wiki ya pili.

Wodi na viingilio vyote vilikuwa vimefungwa kwa kufuli wakati tulipotembelea asasi hiyo.

Hospitali ya Rufaa ya Msambweni huwa inahudumia maelfu ya wakazi wa Kwale kutoka Lungalunga, Vanga, Kinango hadi Samburu.

Wagonjwa waliokuwa wakitegemea hospitali hiyo kwa matibabu sasa wanalazimika kurudi makwao au kutafuta huduma mbadala katika hospitali za kibinafsi zilizo ghali.

“Nilikuja hospitalini kwa sababu mwanangu alipata jeraha kichwani alipokuwa akicheza shuleni na alihitaji matibabu. Nimeambiwa hakuna daktari kwa hivyo nimelazimika kurudi nyumbani au kutafuta hospitali nyingine,” akasema Bi Khadija Hassan.

Alisema hospitali nyingi za kibinafsi ni ghali na wakazi wengi hawawezi kumudu.

Hali sawa na hiyo ilimkumba Bi Mwanahamisi Cheti, mkazi wa Shimoni ambaye alikuwa amesafiri kuenda hospitalini akiwa na maumivu ya jino.

Hali ni hiyo hiyo katika zahanati zaidi ya 60 zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.

Katika kituo cha afya cha Diani, wagonjwa walikosa kuhudumiwa huku ofisi za kituo hicho cha matibabu zikiwa zimebaki mahame.

Mgomo wa madaktari unatokana na malalamishi ya kutopandishwa vyeo na kutolipwa marupurupu ya kupandishwa vyeo kwa wahudumu wa afya yasiopungua Sh16 milioni.

Mgomo huo pia umesitisha utoaji wa chanjo ya corona katika zahanati zilizoathiriwa, licha ya Kwale kuzindua shughuli ya kuongeza utoaji chanjo kwa umma wiki jana.

Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, alisema awali kuwa mgomo wa madaktari unachochewa kisiasa na akatishia kuwa wasiorejea kazini watapigwa kalamu.

Hata hivyo, madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa matibabu wameshikilia kutorudi kazini hadi pale watapokea malipo yao.